Katika hali inayoonesha hana kinyongo kwa kutoteuliwa kuwa mgombea wa ubunge wa jimbo la Lindi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Aliyekuwa mtia nia yakuwa mgombea wa ubunge kupitia CCM katika jimbo hilo la Lindi, Mohamed Utali amesema wana CCM waliotia nia ya kugombea udiwani, ubunge na uwakilishi ambao wanahamia vyama vingine vya siasa baada ya kushindwa kuteuliwa na chama hicho ni waroho wa madaraka na wabinafsi.
Utali ameyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika manispaa ya Lindi.
Utali ambaye kitaaluma ni mwalimu na alikuwa mkuu wa wilaya ya Mmvomero alisema kuhama chama hicho na kujiunga na vyama vingine vya siasa ni ushahidi unaothibitisha kwamba watu hao hawakuwa na mapenzi ya dhati kwa CCM. Lakini pia walikuwa na malengo binafsi ambayo ni kinyume na malengo ya chama hicho tawala.
Alisema mbali na ubinafsi lakini pia ni walaghai kwa wananchi. Akibainisha kwamba nijambo lisilokubalika watu hao ambao waliwaaminisha wananchi kwamba wangewapelekea maendeleo kupitia CCM lakini ghafla baada ya kushindwa kuteuliwa wanajiunga na vyama walivyovisema havifai kuaminiwa.
'' Ubinafsi ni katika sifa isiyofaa kwa kiongozi yeyote. Hivyo kiongozi mbinafsi hata kumuamini kumpa mate yako akatupe, sembuse kumuamini kumpa madaraka au jukumu la uwakilishi!,'' alisema Utali.
Utali ambaye ameahidi atakuwa mstari wa mbele kumnadi aliyeteuliwa kuwa mgombea wa ubunge wa jimbo la Lindi kupitia CCM ( Amida Abdallah) aliwaonya wanachama walioteuliwa kugombea nafasi za udiwani, uwakilishi na ubunge nchi nzima wawadhibiti wapambe wao.
Alionya kwamba wapambe wakiwasimanga na kuwabeza wasioteuliwa inaweza kuwa nisababu ya kuendeleza makundi. Kwahiyo wawaweke karibu na wanachama wasioteuliwa ili chama hicho kipate ushindi.
'' Viongozi wa ngazi zote wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Lindi wahakikishe wanafanya juhudi kubwa ya kutibu majereha yaliyotokana na uteuzi wa wagombea ambayo kwa vyovyote vile tulikuwa hatuwezi kuyaepuka kwani nafasi iliyokuwa inashindaniwa ni moja katika kila jimbo na kata,'' Utali alisisitiza.
Wanachama 19 walijitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama hicho ili wawe wagombea wa ubunge katika jimbo la Lindi. Ambapo kada huyo alikuwa ni miongoni mwa ambao hawakuteuliwa.