Msemaji wa mkutano mkuu wa kitaifa wa chama cha Republian nchini Marekani amesema kuwa kura ya kumchagua tena Rais Donald Trump kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho itaandaliwa faraghani baadaye mwezi huu bila ya kuwepo kwa wanahabari kutokana na janga la virusi vya corona.
Wajumbe 336 wa mkutano mkuu wanatarajiwa kukutana mjini Charlotte katika jimbo la North Carolina tarehe 24 mwezi huu kupiga kura rasmi ya kumteua Trump kuwa mgombeaji wa chama hicho kwa mara nyingine tena.
Vikao vya uteuzi kwa kawaida huwa vinashirikisha wanahabari huku vyama vya kisiasa vikitarajia kutumia fursa ya hafla hizo kusambaza ujumbe wao kwa wapiga kura wengi iwezekanavyo. Iwapo msimamo wa chama hicho utadumishwa, hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa uteuzi wa vyama kutowashirikisha wanahabari katika historia ya sasa.