BAADA kushindwa kufikia muafaka mzuri na beki wao wa pembeni Juma Abdul, uongozi upo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa mabeki wawili Hassan Kessy wa Nkana Rangers na Kibwana Shomari anayeichezea Mtibwa Sugar.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu beki huyo na mkongwe Kelvin Yondani kugomea mkataba baada ya uongozi wa timu hiyo kutaka kuwasajili bila ya ada ya usajili.
Mabeki hao tayari wamewaaga mashabiki wa timu hiyo na kuondoka kwenda kwenye klabu nyingine kutafuta changamoto mpya ya ushindani huku Namungo FC ikitajwa kuwawania nyota hao Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, uongozi wa Yanga kwa kushirikiana na Kampuni ya GSM imeanza mazungumzo na mabeki hao wote wawili tayari kwa kuja kuichezea timu hiyo.
Aliongeza kuwa mabeki hao wote tayari wamepewa ofa za usajili na kama mazungumzo yakienda, basi nyota hao wawili au mmoja atasaini mkataba wa kuichezea Yanga.
“Baada ya kuachana na Abdul, hivi sasa uongozi upo kwenye mazungumzo mazuri na mabeki wawili, Kessy na Kibwana mmoja wapo kati ya hao au wote wawili huenda tukawasajili kama tukifikia muafaka mzuri.
“Wote ni wachezaji wazuri wenye viwango vikubwa na tegemeo katika timu zao, kikubwa tunataka kutengeneza kikosi kitakachokuwa imara na tishio katika msimu ujao,” alisema mtoa taarifa huyo.