HABARI kuwa Lionel Messi anataka kuondoka ndani ya Barcelona imesababisha klabu tatu za Ulaya kuanza kujisogeza kutaka kumsajili.
Raia huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 33, hana makali kama miaka mitano iliyopita lakini hiyo haipunguzi ubora wake na kumfanya kuwa lulu kwa vigogo wengine wa Ulaya.
Timu zinazotajwa kuwa zinaweza kunasa saini kwa asilimia kubwa ya staa huyo ni Inter Milan ya Italia, Manchester City ya England na Paris Saint- Germain ya Ufaransa.
INTER MILAN
Imekuwa na ndoto ya kumsajili staa huyo kwa miaka kadhaa sasa, inadaiwa wameshandaa euro 260m za kumsajili, lengo lao akanogeshe ushindani kwa Cristiano Ronaldo wa Juventus.
MANCHESTER CITY
Kocha Pep Guardiola anatamani kufanya kazi na Messi kwa mara nyingine, ni klabu chache ambazo zinaweza pia kumudu mshahara wa kumlipa wakiwemo Man City.
Guardiola hajabeba ubingwa wa Ulaya tangu alipoondoka Barcelona na hilo ni kama deni kwake, usajili wa Messi unaweza kumuongezea nguvu ili akaungane na rafiki yake, straika wa timu hiyo, Sergio Aguero.
PARIS SAINT-GERMAIN
Kama ni suala la fedha kwao siyo jambo la kuuliza, hivi karibuni waliishia fainali ya Ulaya, wanaamini wakiwa na Messi wataweza kubeba taji hilo.
Pia uwezo wa Neymar na Kylian Mbappe unaweza kumpunguzia majukumu Messi wakiwa uwanjani.