Vinywaji Vinavyoongeza Uzito wa Mwili...
1
October 02, 2021
Hivi umewahi kujiuliza ni kwanini, pamoja na juhudi zote unazozifanya za kujizuia kula baadhi ya vyakula na mazoezi unayoyafanya lakini mwili wako haupungui?
labda kuna kitu ambacho bado hujakitambua kinachosababisha uzito wako kubakia palepale au kupungua kidogo sana.
Uhusiano kati ya chakula na kuongezeka kwa uzito wa mwili pamoja na unene ni mkubwa sana. Jambo hili huwafanya watu kuwa makini na vyakula wanavyokula lakini wanajisahau katika vinywaji wanavyovitumia.
Kama hukuwa unafahamu, basi leo nikufahamishe kuwa vinywaji unavyotumia vina mchango mkubw sana katika kuongezeka kwa uzito wa mwili wako pamoja na unene.
Hivi ni baadhi ya vinywaji vinavyoongeza uzito wa mwili lakini tumekuwa tukivipuuzia;
Chai na kahawa
Asubuhi inakuwaje kama usipopata kikombe kimoja cha chai ya moto? wengine mpaka saa 4 asubuhi hutaka kujipasha kwa kikombe cha chai ama kahawa. Wapo waliojizoesha hata kunywa chai ama kahawa nyakati za jioni.
Ni kweli kuwa majani ya chai yana virutubisho muhimu na vyenye msaada mkubwa katka mwili wako. lakini unapoongeza kijiko kimoja au viwili vya sukari hapo ndipo unapoongeza kiwango cha kalori katika mwili wako.
Kikombe kimoja kwa siku siyo vibaya, lakini unapojiwekea mazoea ya kunywa vikombe vinne au vitano vya chai hapo kuna vijiko 8 mpaka 10 vya sukari, hivyo unazidisha uwezekano wako wa kunenepa.
Kwa wanywaji wa kahawa, haswa wale wanaokunywa kahawa zilizotengenezwa katika mighahawa ya kahawa ‘Coffee shops’ wao huweka maziwa mazito ili kuzifanya kahawa zao kuwa na mvuto. Hapa siyo tu unaongeza kiwango cha sukari, bali pia unaongeza kiwango cha mafuta ‘fat’ yatokanayo na maziw yanayowekwa katika kahawa hiyo.
Vilevi
Watu wengi hudhani kuwa kama wakiacha kunywa vilevi vinavyotengenezwa na ngano basi wako salama. Jambo hili liko mbali na ukweli kwani hata vinywaji vingine vikali ukiwamo mvinyo na ‘spirits’ vinakuwa na kiwango kikubwa cha kalori ambazo kama zikiingizwa kwa wingi katika mwili wako basi kuna uwezekano mkubwa wa wewe kuwa mnene.
Mfano glasi moja ya mvinyo ina kalori sawa na kipande kimoja cha keki, hivyo usijidanganye kuwa ukitumia vilevi bila mpangilio hautonnepa.
Soda
Hakuna jambo linalouburudisha mwili kama kujipatia soda ya baridi kabisa wakati wa joto kali. Wengi wamekuwa na tabia hii hasa wale wanaoishi katika mazingira ya joto. Jambo ambalo unapaswa kujua ni kwamba soda yenye ujazo wa 500ml (nusu lita) ina kiwango cha kalori 200 ambazo ni sawa na 10% ya kiwango cha kalori anachopaswa kutumia mtu mzima kwa siku moja.
Kiwango cha kalori unachokipata kutoka katika soda moja ni sawa na kiwango utakachokipata katika Ugali na Mchicha. Ubaya ni kwamba kwenye soda unapata maji na sukari tofauti na kwenye chakula ambapo unapata virutubisho tofauti tofauti.
Sharubati ya matunda (Fruits juice)
Sharubati imekuwa ikitumiwa zaidi na watu wengi kama mbadala wa vinywaji vingine kama vile soda, kwani inaaminika kuwa na faida katika mwili tofauti na soda zenye kemikali zinazoweza kupelekea athari mwilini. Sharubati kwa kawaida ni nzuri kwa afya ila nyingi zinazopatikana huwa zimeongezwa sukari.
Sharubati zinazotengenezwa viwandani zina 10% tu ya kiwango cha matunda na vilivyosalia ni maji pamoja na sukari. Vitu hivi vinachangia sana katika kunenepa kwa mwili kama vitatumiwa mara kwa mara.
Tags
Kwa kuchangia tu kahawa si tatizo wala chai, unajua huu ni mitandao wa watu wengi nadhani mnapotoa ushauri juu ya matumizi ya vitu fulani kuhusiana na masuala ya afya za watu ni bora kuwe na uthibitisho wa kisayansi kuthibitisha madai hayo au la sivyo mtakuwa mnapotosha jamii. Au kuwe na ufafanuzi katika mada husika inayoelezea au kuwajulisha wasomaji kwamba madai hayo ya madhara au faida ya kutumia kitu fulani hayana uthibitisho wa kisayansi. Tatizo sio chai wala kahawa tatizo ni..SUKARI (Sugar or sugary products) ukiiendekeza sukari au ukiendekeza kutumia vilaji vya sukari kwa kiwango kikubwa basi matokeo yake ni kukuletea madhara mwilini na ni kutokana na uthibitisho wa wataalamu wa afya. Pengine kwa angalia matatizo ya unene wa hatari unaoambatana na magonjwa ya moyo na sukari kwa kwetu Tanzania. Tunatakiwa kuwa makini katika matumizi ya vyakula vya mafuta. Na hasa kutupia macho zaidi katika aina za mafuta tunayotumia kutayarishia vyakula tunavyokula yana ubora wa aina gani? Mfano mayai yaana mafuta ya asili ndani yake tayari, tena mengi tu sasa unapotumia mafuta kuyapika sawa na kuongeza sukari kwenye asali. Au baadhi ya samaki tayari wanamafuta ya asili tena dawa sasa unapotumia mafuta tena mafuta yenyewe ya hovyo kuwapika sawa na kunyunyuzia vimelea vya maradhi katika dawa ya kutibu maradhi . Maziwa,mayai,Nyama hivi vitu ni hatari kwa afya ya mwanadamu ikiwa muhusika atatumia vyakula hivi kupita kiasi bila ya mpangilio mzuri wa mazoezi ya mwili. Utumiaji wa mayai, nyama na maziwa ili ulete tija mwilini unatakiwa uwe wa kiasi. Lakini cha msingi kwa mwanadamu hakuna chakula bora cha mwili na msingi wa uzima na utimamu wa mtu kiafya kama mazoezi ya mwili.
ReplyDelete