Kati ya jambo ambalo unatakiwa kuwa nalo makini sana ni pale unapotaka kutoa msaada. Inaweza ikawa ni ukweli unaouma, lakini iko hivi si kila mtu anahitaji msaada wako, wapo watu ambao msaada wako hawataki ila wewe unajipendekeza tu kwao.
Si kwambii usitoe msaada, toa msaada ila kwanza anza na kuchunguza, hutakiwi kutoa msaada wowote hovyo hovyo kama unagawa karanga. Hebu waangalie matajiri misaada yao wanatoa hovyo kwani? ni watu makini sana katika kutoa misaada yao.
Hata wewe unatakiwa kuwa hivyo, pamoja na kwamba wewe unaweza ukawa ni mtu mkarimu, lakini ukarimu wako usipitilize na kuwa matatizo kwako kwa kutoa msaada ambayo itakuumiza wewe na kukufanya ujute, kwa nini ulitoa msaada.
Pengine naomba nikuulize, hujawahi kuona watu wakilalamika au wakisononeka kwa sababu ya kutoa misaada yao ambayo baade iliwageukia? Wapo watu wa namna hiyo ambayo misaada yao iliwatokea puani na kuwa maumivu makubwa.
Kama hujanielewa vizuri naomba nikwambie hivi, si watu wote wanahitaji msaada wako, chagua wale ambao wanahitaji msaada wako kweli na wape. Utajuaje hilo, naomba nikwambie watu ambao hutakiwi kuwapa msaada wako hata iweje.
1. Usitoe msaada kwa watu ambao hawastahili kupata msaada wako.
Naamini kabla hujatoa msaada wowote, kuna watu ambao unaona kabisa kutokana na vigezo ulivyoweka unasema watu hawa wanastahili msaada wangu. Kama unaona watu hawa hawajatimiza vigezo, usitoe msaada huo.
Kwa mfano, tuchukulie umeanzisha huduma ya aina fulani iwe semina au kitu chochote na unataka wartu walipie ndio wapate huduma hiyo. Inapotokea baadhi ya watu wameshindwa kulipia usitoe huduma hiyo kwao hata kidogo.
Hata inapotokea wamekujia na maombi ya uwape huduma bure kataa, maana hao hawastahili msaada wako. Tatizo la watu wengi wanapenda sana kuwanyonya watu wengine, na hawataki kuingia gharama yoyote ile wanataka vya bure tu.
Kwa hiyo unapoona watu hawako tayari kufata vigezo, basi ujue watu hawa hawataki kulipa gharama na kama watu hawako tayari kulipa gharama na msaada wako pia wanauona si kitu na ndio maana hata gharama unazoweka hawalipi.
Usiwe rahisi kutoa msaada, na kama umeamua kutoa msaada wa bure hakikisha kuna namna unayofaidika kwenye msaada hupo pasipo watu hao kujua au hata kwa kujua. Kikubwa usikubali kunyonywa na ukabakizwa mweupe kwa sababu ya msaada.
2. Usitoe msaada kwa watu ambao hawako tayari kupokea msaada wako
Kuna wakati unaweza ukawa una nia nzuri tu ya kutoa msaada, kwa mfano, kuwashauri rafiki zako au ndugu zako juu ya kufanya mradi wa aina fulani ambao ni mzuri na utawatoa kiuchumi toka sehemu moja na kwenda nyingine.
Lakini nikwambie hivi, watu hao ambao unakuwa umepanga kuwapa msaada huo kama hawako tayari kuupokea na wala hawana hamasa na shauku ya kuupokea msaada huo, inakuwa ni sawa na kazi bure na tena watakuwa adui zako wakubwa
Hapa kitu unachotakiwa kuwa nacho makini ni kuangalia usitoe masada wowote ule kwa kujipendekeza ili uonekane ni mwema. Dunia na watu wake hawana shukrani, unaweza ukajuta sana kwa nini ulimsaidia sana mtu huyu au watu wale.
Ni jambo la kusikitisha na kupoteza muda wako sana kama unawasaidia watu ambao hawasaidiki. Hapa ndipo umuhimu wa kuchunguza mazingira watu unawaotaka kuwasadia wanataka msaada wako au hawaututaki hata kuusikia kwenye masikio yao.
Kikubwa kwako hapo kaa kimya, kama kuna watu wanahitaji msaada wako kweli wa hali na mali najua watakuja kwako lakini si kutoa msaada kwa watu ambao hawako tayari kuupokea na wala hawana shukrani, achana na hiyo baishara mara moja.
Kwa kuhitimisha makala hii ieleweke hivi, hao ndio watu ambao hutakiwi kuwapa msaada, lakini hata hivyo na wewe usitoe msaada kama huna uhakika msaada huo utaufanikisha kwa asilimia kubwa kama inavyotakiwa iwe.
Mazingira yoyote yatakayopelekea wewe ukashindwa kufanikisha msaada utajenga uadui mkubwa sana kati yako wewe na yule ambae ulikuwa umeamua kumpa msaada tena kwa nia iliyo njema, kuwa makini katika hilo.
Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatimia.