MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA),imewataka wananchi kuondoa hofu juu ya upungufu wa mafuta ya taa uliopa hivi sasa na badala yake kuwa watulivu.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu upungufu wa mafuta ya Taa nchini huko katika Ukumbi wa Ofisi ya ZURA ilioko Maisara Mkuu wa Kitengo cha uhusiano Khuzaimat Bakari Kheir amesema changamoto ipo kwa baadhi ya vituo tangu mwisho wa mwezi wa JULY 2020.
Amesema hali hiyo ilitokana na mafuta ya Taa kutonunuliwa kwa muda wa miezi mitatu kutoka nje ya Nchi kwa sababu ya mripuko wa maradhi ya corona (Covid 19).
Hata hivyo alisema kutokana na hali hiyo ZURA ilifanya jitihada ya kuzungumza na Kampuni ya PUMA ili kuzipatia kampuni nyengine mafuta hayo na yalipatikana hadi ilipotokea ajali ya moto katika kampuni hiyo tarehe 21 Julai 2020.
Hivyo kutokana na kwa ajali hiyo ZURA kwa kushirikiana na Kampuni ya United Petrolium imechukua hatua ya kwenda kuchukua mafuta ya taa kutoka Nchi jirani ya Kenya (Mombasa )kwa ajili ya kuondoa upungufu wa mafuta ya Taa.
Amesema hivi sasa meli ya United Spirit imeshawasili katika Bandari ya Mombasa tayari kwa ajili ya upakizi wa mafuta ya taa, baada ya ushushaji wa mafuta kwa kampuni hiyo meli hiyo inatarajiwa kupakia Lita Laki sita (600,000) za mafuta ya taa leo na kufika Zanzibar tarehe 12 Agosti 2020.
Pia Khuzaimat amesema ZURA inawaomba radhi wananchi kwa usumbufu uliojitokeza na kueleza kwamba inafatilia kwa karibu changamoto na kuhakikisha hali ya upatikanaji wa mafuta ya taa inarejea kama kawaida nchini.
“Mamlaka inawaonya wamiliki wa vituo vya mafuta kutouza kwa bei ambazo sio rasmi hatua kali zitachukuliwa kwa atakaekwenda kinyume”, alitoa msisitizo Mkuu wa kitengo hicho.
Pia amesema bei za bidhaa za mafuta ya Petrol na Dizel katika mwezi wa Agosti , 2020 zimepanda , wakati mafuta ya taa imeshuka ikilinganishwana mwezi wa Julai 2020 kutokana kubadilika kwa wastani wa bei za uuzaji wa bidhaa hizo katika soko la dunia pamoja na soko la ndani kwa kupitia bandari ya Dar-Es-Salaam.