Maelfu ya wanawake waliandamana katika mji mkuu wa Belarus, Minsk hapo jana wakipeperusha bendera, maua na maputo katika mfululizo wa maandamano ya hivi punde dhidi ya serikali ambayo yameikumba nchi hiyo tangu kufanyika kwa uchaguzi wa urais uliokumbwa na utata mwezi huu.
Wanawake hao waliandaa maandamano hayo waliyoyaita maandamano ya umoja na kutoa wito kwa Lukashenko na serikali yake kujiuzulu.
Rais Alexander Lukashenko amekanusha madai ya upinzani kwamba aliiba uchaguzi huo wa Agosti 9 kurefusha uongozi wake wa miaka 26.
Barabara ambazo zilitumika katika maandamano hayo zilifungwa na polisi na vikosi vya ulinzi.
Maandamano madogo kama hayo yalifanyika katika miji mingine.
Lukashenko amesema kuwa waandamanaji hao wanafadhiliwa na mataifa ya Magharibi na kuishtumu jumuiya ya kujihami ya NATO kwa kuongeza vikosi katika mipaka yake madai yaliyokanushwa na jumuiya hiyo.