Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema leo kwamba Lebanon inahitaji serikali inayoweza kupambana dhidi ya rushwa na kuanzisha mageuzi.
Maas ameyasema hayo wakati akizuru bandari ya Beirut, kulikotokea mlipuko mkubwa ambao ulisababisha vifo vya watu wasioupungua 171, na kuwajeruhi karibu 6,000.
Maas ametoa hundi ya zaidi ya euro milioni moja kwa shirika la Msalaba Mwekundi, ikiwa ni sehemu ya msaada jumla wa kiutu wa euro milioni 20 kutoka Ujerumani.
Msaada wa kimataifa umepelekwa nchini Lebanon, lakini mataifa ya kigeni yameweka wazi kwamba hayatatoa pesa kwa serikali ambayo inashutumiwa na raia wake kwa ufisadia uliokithiri.
Hii leo Lebanon imewazika wahanga zaidi wa mlipuko huo, huku timu za uokozi za Lebanon na mataifa ya kigeni zikiendelea kufukua vifusi kutafuta miili zaidi ya watu ambao bado hawajatolewa maelezo.