KLABU ya Yanga kupitia Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambao ni wadhamini wa Klabu hiyo, Hersi Said imethibitisha kuwa wamebaki wachezaji wanne kusajiliwa ili kufunga kazi ya usajili.
Hersi amesema kuwa, wamemaliza usajili wa wachezaji wa ndani ambapo wa mwisho ni winga wa kushoto, Farid Mussa aliyesaini mkataba juzi.
“Tunahitaji washambuliaji wawili wa kati, tayari tuna mmoja mpaka sasa Yacouba (Sogne) ambaye ameshasaini mkataba wa miaka miwili, kuna haja ya kuwa na winga wa kulia ambaye atakuja kuongeza kasi kule mbele. Kuna mbadala wa Tshishimbi (Papy) atakayekuja kucheza kama kiungo mkabaji.
“Tulikuwa tunafikiria tuipeleke timu yetu (Yanga SC) sehemu maalum nje kwa ajili ya maandalizi, lakini mpaka sasa hatujamtangaza kocha mpya na mchakato huenda ukakamilika wiki hii.
“Utaona pia muda si rafiki sana uliosalia kabla ya kuanza ligi, ni mchache na bado hata wachezaji wote hawajakutana kama timu, tuna tamasha la Wiki ya Mwananchi, hivyo uwezekano wa timu kuandaliwa hapahapa ndani ni mkubwa,” amesema Eng. Hersi