HAYAWI hayawi sasa yamekuwa! Yule kikongwe Nasi Muruo (99) aliyekuwa akitafuta haki yake kwa zaidi ya miaka 40, sasa amelipwa kiasi cha shilingi milioni 206.5, zikiwa ni malipo ya fidia ya ardhi yake kutoka kaya 76 zilizoamriwa na serikali kumlipa.
Akizungumza na mwandishi wetu mwishoni mwa wiki iliyopita, Muruo ambaye ni mkazi wa Sinoni, jijini Arusha alisema jumla ya kaya 44 zimekamilisha malipo ya shilingi 206.5 milioni, huku kaya 32 zikiwa zimeanza kumlipa shilingi 57.6. milioni.
“Lakini kuna kaya 22 ambazo hazijalipa kabisa kiasi chochote na zinadaiwa shilingi 56.4 milioni,” alisema bibi huyo.
“Nazishukuru kaya ambazo zimenilipa na zilizoanza kunilipa. Namshukuru Rais John Magufuli na Waziri wa Ardhi, Willium Lukuvi kwa sababu nimeanza kupata haki yangu baada ya kuitafuta kwa miaka 43,” alisema bibi Muruo.
Naye mjukuu wa bibi huyo, Obedi Saiteru alisema wanaomba familia iliyosababisha mgogoro huo kuondolewa eneo hilo kwa kuwa imeanza kampeni za kushawishi watu wasikamilishe malipo na waendelee kung’ang’ania ardhi ya bibi yake.
Alisema familia hiyo hawamo katika kulipa fidia na hawahitaji kufanya hivyo kwa sababu wamesababishia matatizo hayo licha ya bibi yao (Murua) kushinda kesi mahakamani, hivyo kwa sasa wanachotaka ni familia hiyo iondoke mara moja au iondolewe na serikali. Aliitaja familia hiyo kuwa ni ya marehemu Edward Lenjeshi.
Mjane wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Vicky, alipohojiwa kuhusu madai ya kushawishi watu wasilipe au wasihame eneo hilo, alikanusha.
“Siwezi kupingana na maagizo ya serikali ya kutaka bibi huyo kulipwa fi dia au kuzuia watu wasihame,” alisema mama huyo.
Sakata la bibi huyo la kudai kudhulumiwa, liliingiliwa kati na Rais Magufuli na kuamuru bibi Nasi Muruo arejeshewe ardhi yake baada ya kudhulumiwa mwaka 1977. Bibi huyo baada ya kudhulumiwa, alikwenda mahakamani na alishinda kesi ya kurejeshewa ardhi hiyo mwaka 1979, lakini ikashindikana.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi Agosti 28 mwaka jana alizitaka kaya 110 zilizojenga kwenye ardhi ya bibi huyo, kumlipa fi dia ya jumla ya shilingi 519.3 milioni kulingana na ukubwa wa kila nyumba, vinginevyo zitabomolewa. Alielekeza kuwa, kila mita moja ya mraba, inapaswa kulipwa shilingi 20,000.