Majaribio ya kitabibu ya moja kati ya chanjo ambayo yamepiga hatua kubwa kupambana na ugonjwa wa COVID-19, inayotayarishwa na kampuni ya madawa ya AstraZeneca na chuo kikuu cha Oxford, yamesitishwa kwa muda.
Hii ni baada ya mtu aliyejitolea kufanyiwa majaribio kuanza kuonesha dalili za ugonjwa ambao haufahamiki.
Wakati mabilioni ya watu duniani kote bado wanateseka kutokana na kuzuka kwa janga hilo la virusi vya corona pamoja na idadi ya vifo duniani kukaribia laki 9, mbio duniani kote kwa ajili ya kupatikana chanjo zinaendelea, ambapo makampuni tisa tayari yamo mwishoni mwa awamu ya tatu ya majaribio.
Maambukizi duniani kote hadi sasa ni zaidi ya watu milioni 27, na zaidi ya watu 890,000 wamefariki kutokana na ugonjwa huo. Urusi tayari imeidhinisha chanjo , na utafiti uliochapishwa katika jarida la kitabibu la Lancet wiki iliyopita umesema wagonjwa waliohusishwa katika majaribio ya mwanzo walipata chembe zinazokinga mwili, na hakuna matatizo yaliyotokea. Lakini wanasayansi wanatahadharisha kuwa majaribio hayo ni madogo mno.
Msemaji wa kampuni ya madawa inayotengeneza chanjo hiyo AstraZeneca amesema katika taarifa jana kuwa “tunasitisha kwa hiari chanjo hiyo kuruhusu hatua za kuangaliwa upya data za usalama na kamati huru.
“Hii ni hatua ya kawaida ambayo inapaswa kutokea wakati kuna uwezekano wa ugonjwa ambao haufahamiki katika moja kati ya majaribio, wakati unachunguzwa, na kuhakikisha tunaendelea uhalali wa majaribio.
Kampuni hiyo imesema kuwa katika majaribio mengi, magonjwa baadhi ya nyakati yanatokea kwa bahati lakini ni lazima kufanyiwa uchunguzi huru.
AstraZeneca haikutoa taarifa zaidi, lakini tovuti ya taarifa za kitabibu ya Stat News, ambayo iliripoti kwanza ugonjwa wa mtu huyo aliyejitolea kufanyiwa majaribio, imenukuu chanzo kikisema ugonjwa huo umehusisha hali mbaya ya mwili kupambana na chanjo hiyo.
“Wakati bila shaka hizi si habari nzuri, kumbuka kwamba uchunguzi kamili wa hali hiyo ni sehemu ya majaribio ya kiwango kikubwa na muhimu kuhakikisha uaminifu katika chanjo yoyote.
Hata hivyo itakuwa na maana kwamba matokeo yatacheleweshwa,” mtaalamu wa magonjwa ya maambukizi kutoka chuo kikuu cha Harvard Bill Hanage aliandika katika ukurasa wa Twitter.
Kwa mujibu wa Stat News, mgonjwa huyo aliyejitolea kufanyiwa majaribio ya chanjo ana uwezekano wa kushiriki katika awamu ya 2 na ya tatu ya majaribio nchini Uingereza.
Barani Ulaya wasi wasi unaongezeka juu ya kurejea kwa virusi, ambapo Ufaransa inabana vizuwizi, kesi za maambukizi nchini Uingereza zikiongezeka na shule zinafunguliwa tena katika kanda ya Ulaya.
China, wakati huo huo, imeonesha chanjo yake iliyotengenezwa nchini humo kwa mara ya kwanza katika maonesho ya biashara mjini Beijing wiki hii, na maafisa wanamatumaini kuwa chanjo hiyo itaidhinishwa kwa ajili ya matumizi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.