Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli amewataka Watanzania kufanya uchaguzi kwa makini na kuepukana na sera zinazotaka kuligawa Taifa kwa kuleta mfumo wa majimbo.
Akizungumza na wakazi wa Urambo mkoani Tabora ikiwa ni muendelezo wa kampeni za chama hicho amesema kuwa kuna baadhi ya vyama havina sera na kwamba vinataka kulirudisha taifa nyuma.
Dkt. Magufuli amesema kuwa wakati wa kutafuta uhuru wa nchi, endapo Mwalimu Julius Nyerere angeigawa katika majimbo, Tanzania isingekuwa hapa ilipo leo.
“Mmesikia kwenye Kampeni za hivi karibuni mnaambiwa yatatengenezwa Majimbo,Tanzania itagawanywa ni Chama fulani kina sera yake hiyo ya kuigawanya Tanzania katika Majimbo ya Utawala, ukishatengeneza Majimbo katika Nchi huo ndio mwanzo wa mfarakano
“Ukishagawanya Nchi katika Majimbo ni mwanzo wa ufarakano kwasababu kila Jimbo litakuwa linajitegemea lenyewe likiwa masikini linakuwa masikini wa kutupwa, Nyerere alipokuwa akiomba Uhuru wa Taifa hili angeligawa kwenye Majimbo tusingefikia hapa
“Tanzania tuna Makabila zaidi ya 121, Nyerere alituweka Watanzania kama Taifa moja, tangu 1961 hatujaingia mfarakano kati ya Kabila na Kabila, Dini na Dini, Maeneo, sitaki nitoe mifano ya baadhi ya Nchi ambazo ziliingia kwenye mtego wa Majimbo na wamefarakana
“Mngekuwa na Jimbo lenu hapa labda Jimbo la Tabora na wapi hizi Barabara tungetoa wapi hizo Bilioni 567, fedha hizi hazikutolewa na Tabora ni Tanzania nzima imeshiriki, Arusha, Mwanza, DSM wamechangia, kataeni mbinu za kutugawa kwa kusema watagawa Majimbo”- Amesema Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM Dr. John Magufuli leo akiwa Urambo Tabora.