Madagascar iliwavutia wengi na kuangaziwa sana Aprili taifa hilo lilipotangaza kwamba lilikuwa limevumbua dawa ya corona kutoka kwa mmea.
Dawa hiyo iliyokuwa imeandaliwa kama kinywaji ilitengenezwa kwa kutumia mmea wa artemisia, na rais Andry Rajoelina aliipigia debe sana.
Kufikia sasa bado hakuna ushahidi kwamba mmea huo - ambao kemikali zake huweza kudhibiti malaria - unaweza kutibu Covid-19, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Tunafahamu nini kufikia sasa kuhusu mmea huu na nguvu zake?
Mmea huu unatoka wapi?
Mmea huo kwa jina kamili huitwa Artemisia annua na asili yake ni bara Asia, lakini hukuzwa katika maeneo mengi duniani yenye joto na jua.
Mmea huu umekuwa ukikuzwa katika baadhi ya mataifa ya Afrika mashariki zikiwemo Kenya na Tanzania.
Mmea huu umetumiwa kama tiba ya kiasili nchini China kwa zaidi ya miaka 2,000 kutibu magonjwa mengi, ukiwemo ugonjwa wa malaria. Hutumiwa pia kupunguza maumivu na kudhibiti homa.
Kwa Kiingereza huitwa sweet wormwood au annual wormwood, na baadhi ya watu wamekuwa wakiutumia kwa sababu mbalimbali kama tiba, na hata kuongezwa kwenye vinywaji.
Artemisia inaweza kudhibiti Covid-19?
Rais Rajoelina wa Madagascar mwezi Aprili mwaka huu alisema majaribio yalikuwa yamefanyiwa tiba ya Covid-Organics iliyotengenezwa kwa kutumia mmea huo na kwamba majaribio hayo yalionesha mafanikio.
Alirudia madai hayo mwezi huu wa Septemba.
Lakini taifa lake halijatoa ushahidi wowote wa kisayansi hadharani kuthibitisha madai hayo.
Aidha, viungo halisi vilivyo kwenye dawa hiyo ya kinywaji kwa jina Covid-Organics havijulikani hasa, ingawa serikali ilisema 60% inatokana na mmea wa artemisia annua.
Kiwango hicho kingine kinatokana na mimea mingine ya kiasili.
Madagascar pia imekuwa ikitengeneza tembe za Covid-Organics na hata dawa ya kudungwa kwa kutumia sindano. Rais Rajoelina anasema majaribio ya hiyo ya dawa ya kuchomwa mwilini kupitia sindano yanaendelea.
Wanasayansi kutoka Ujerumani na Denmark wamekuwa wakifanyia majaribio kemikali kutoka kwa mimea ya artemisia annua, na walisema mmea huo ulionyesha mafanikio dhidi ya virusi vya corona kwenye maabara.
Utafiti huo - ambao haujahakikiwa na wanasayansi wengine - ulibaini kwamba kemikali za mmea huo zilionyesha sifa za kukabiliana na virusi hivyo zilipotolewa kwa mmea huo kwa kutumia maji au kilevi.
Watafiti hao kwa sasa wanafanya kazi kwa pamoja na Chuo Kikuu cha Kentucky kufanyia majaribio mmea huo kwenye binadamu.
China pia imekuwa ikiufanyia majaribio mmea huo.
Na nchini Afrika Kusini, kuna wanasayansi wanaofanyia majaribio mmea wa artemisia annua na mmea mwingine unaokaribiana sana na huo - artemisia afra - kubaini iwapo unaweza kufanikiwa kutibu Covid-19. Utafiti huo unafanyika katika maabara lakini hakuna matokeo yoyote yaliyotolewa kufikia sasa.