BAO la kiungo wa Yanga, Mkongomani Mukoko Tonombe alilofunga kwenye mechi na Kagera Sugar limewakuna wadhamini wa timu hiyo Kampuni ya GSM kwa kufunguka kuwa ni faraja kwao kutokana na kuanza kupata kile walichokitarajia.
Mabosi hao wameongeza kuwa bao hilo sambamba na mengine yaliyofungwa kwenye mechi zao zilizopita yamewafanya waone kile ambacho walikifanya kwenye wakati wa usajili kikianza kurudi katika kikosi hicho.
Tonombe juzi Jumamosi alifunga bao pekee dhidi ya Kagera Sugar ambalo limewafanya Yanga kufikisha pointi saba baada ya kucheza mechi tatu.
Mabao mengine yalifungwa na Lamine Moro kwenye ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City na Mghana Michael Sarpong wakati wa sare ya bao 1-1 na Prisons.
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said amesema kuwa kutokana na matokeo hayo yameanza kuwapa faraja kwao kwa kuona walichokipanda katika wakati wa usajili kinaanza kulipa ndani ya kikosi hicho.
“Ni faraja kubwa kuanza kupata matokeo baada ya kile ambacho tulitarajia kukifanya msimu huu. Timu yetu tuliijenga na tuliangalia kufanya makubwa kwenye kila idara ikiwa ni kuifanya timu irudi kwenye ubora.
“Tunachotaka ni kuendelea kupambana zaidi kwa ajili ya kufanikisha ndoto za kuwa mabingwa kwa msimu huu na bado tunaona kikosi hakijawa sawa kikiwa kamili zaidi kwa maana wakijuana basi tutakuwa na uwezo wa kufanya makubwa kuliko ilivyo kwa sasa,” alimaliza Hersi