Gwajima; Halima Mdee Njia Panda

 


JIMBO la Kawe linawaka moto hivi sasa kwa kampeni za kukata na shoka, kati ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee.

 

Wote wawili ni watu wenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja na wanajua kuelezea kile wanachokiamini, hivyo uamuzi kubaki kwa wapiga kura Oktoba 28 mwaka huu.

 

Halima Mdee ni mwanasiasa na Askofu Gwajima ni mchungaji wa roho za watu ambaye kwa bahati mbaya sana, atakuwa na kazi ngumu ya kuwa mwangalifu ili asiingie katika mtego wa kuchanganya siasa na dini kama inavyodaiwa.

 

Askofu Gwajima amekuwa moja ya watu maarufu na gumzo kubwa sana nchini. Aina hii ya watu wapo duniani kote. Mtu wa namna hii unapoanza naye vita ya kushindania jambo fulani, unapaswa kwanza kuchukua muda mrefu kujichunguza wewe kwanza kabla hujaanza kumchunguza yeye na kuangalia udhaifu wake.

 

Tumekuwa tukimuona Askofu Gwajima mara kadhaa akisimama kuzungumza anachoamini pasipo kuumauma maneno.

 

Tuliwahi kumuona au kumsikia akimsema aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, tulimuona au kumsikia akiisema serikali iyopita kwa ujasiri na kusababisha kupata matatizo kadhaa, ambayo wengine walisema ni kutokana na hayo aliyokuwa akiyafanya.

 

Miaka ya nyuma alikuwepo Mchungaji Christopher Mtikila, huyu alikuwa na roho kama ya Askofu Gwajima; alizungumza alichoamini pasipo kujali anayemsema au jamii kubwa inayomzunguka ina aamini nini juu ya mtu anayemsema, na Askofu Gwajima ni hivyo hivyo.

 

Aliwahi kukosana na kuwa kama simba na paka na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pale alipomtaja kuwemo katika kundi la kuchunguzwa kutokana na kuhusishwa na madawa ya kulevya, Waswahili wanasema alitoa povu.

 

Watu wa namna hii huongea yale ambayo wengine hawawezi kuongea, huamini kuwa wao ni chachu katika jamii fulani kwa maana ya kuwa wana mchango mkubwa sana. Msimamo wa Askofu Gwajima ni msimamo wa nyundo. Hii ni hulka ya watu ambao wao huamini katika kugonga kila ambacho kitakuwa kimewekwa chini yao.

 

Askofu Gwajima huwezi kumnyamazisha kwa kumpa vitisho, unatakiwa kupambana naye kwa hekima sana na maarifa kama unataka kumvaa.

 

Ukimtisha, yeye huongeza mapambano ya kupigania haki, huyu ni aina ya watu ambao unaweza ukadhani ni wadogo sana lakini wana ushawishi fulani katika jamii na inawezekana, ndiyo maana Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, ikaamua kumteua akapambane na Halima Mdee katika jimbo la Kawe.

 

UWAZI lilibahatika kukutana na Askofu Gwajima mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Mlimani Park na alikuwa na haya ya kusema kuhusu kampeni zake za ubunge.

 

“Mimi nitashinda asubuhi sana kwa sababu kazi yangu ni kushughulika na watu. “Nimekuwa nikifanya kazi za kijamii tangu siku nyingi hata kabla sijawa na wazo la kugombea ubunge.

 

“Mimi sijagombea ubunge kwa sababu ya maslahi, yaani kupata mshahara mnono kwa sababu mimi levo hiyo, nimeshapita,” alisema Gwajima.


Swali: Vipi kuhusu changamoto za barabara jimboni kwako?


Askofu Gwajima: Nitashughulikia kwa urahisi sana. Nitanunua greda na katapila kwa fedha zangu na kuwa mali ya Jimbo la Kawe, hivyo tatizo hilo litakuwa historia.


Swali: Vipi kuhusu kuchanganya siasa na dini?


Askofu Gwajima: Viongozi wa dini hawawezi kujitenga na siasa, huwezi kutenganisha siasa na dini, kwa sababu siasa inahusu watu na dini inahusu watu. Kwa hiyo ni vitu vinavyotegemeana, watu wanaosema kwamba viongozi wa dini wakijihusisha na siasa ni kupotoka, si kweli.

 

Kabla hajawa na wazo la kugombea ubunge, anasema aliwahi kuchimba visima vya maji kwenye misikiti mitatu, na kutawanya maji kwa watu zaidi ya 200 katika Jimbo la Kawe. Alisema akiwa mbunge, atawatetea wananchi wa Kawe na hakutakuwa na mtu wa kumzuia.

 

HALIMA MDEE


Aliyekuwa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ameamua  kupambana na CCM na safari hii akiumana na Askofu Gwajima kugombea ubunge katika jimbo hilo. Halima mwaka jana amechaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha).

 

Halima Mdee anastahili pongezi nyingi tu, kwani pamoja na ‘kuandamwa’ mara kwa mara na kesi nyingi, pia amekuwa akisumbuliwa na aliyekuwa Spika Job Ndugai, huku akikosa ‘Ushirikiano’ wa Serikali, lakini bado tu amejitahidi kufanya kazi jimboni.

 

“Baada ya CCM kumpitisha Askofu Gwajima, nina uhakika nitashinda uchaguzi tena kwa kura nyingi zaidi safari hii kuliko ilivyokuwa mwaka 2015,” anatamba Mdee.

 

“Ukiacha watu kuichoka CCM, Gwajima bado ataponzwa na kauli zake ambazo pia zinapatikana mitandaoni, na uzuri hapa Dar wenye smartphone ni wengi, hivyo itakuwa rahisi watu ku-share clips zake na kufanya aliyoyasema, hasa yale yenye element za udini, kuwafikia watu wengi zaidi na hivyo kumgharimu,” anasema Ashura Mohamed, kada wa Chadema.

 

Halima Mdee alisema sababu nyingine itakayochangia Gwajima ashindwe, ni kutokuwa chaguo la wana-CCM, bali amekuwa chaguo la viongozi wa juu wa CCM, kwani hakushinda katika kura za maoni, hivyo ni wazi wako baadhi ya wanaCCM ambao hawatampigia kura.

 

“Waumini wa Gwajima ni sehemu ndogo sana ya wakazi na wapiga kura wa Jimbo la Kawe, hivyo advantage ya yeye kuwa kiongozi wa dini ni ndogo sana kumbeba bila kusahau ukweli kuwa, Watanzania hawana utamaduni wa kuchagua mtu kwa sababu tu ni kiongozi wa kidini,” anasema Mdee.

 

Halima Mdee amesaidiwa na Tundu Lissu kupigiwa debe na mwitikio wa sera anazonadi Lissu na chama chake miongoni mwa wananchi, ni mkubwa.

 

“Mara nyingi wakati wa kampeni akina mama hujazwa hofu kuwa iwapo watachagua upinzani, basi vita itatokea na wao wataachwa wakiteseka na watoto. Bawacha wanajua hilo na wapo kazini kusaidia kuelimisha wanawake wenzao,” anasema Halima.

 

Kutokana na maelezo hayo, ni wazi kwamba Halima Mdee na Askofu Gwajima wapo njia panda na hadi sasa, haijajulikana nani ataibuka kidedea katika jimbo hilo la Kawe.


MAKALA; ELVAN STAMBULI, UWAZI

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad