*NANI AJUAYE KESHO?*
Mwaka 2005 Diamond alisafiri kwenda Tanga kuomba kuperform kwenye show ya Q-Chilla. Mabaunsa wakamtimua. Alipojaribu kuwaelewesha wakambeba juu juu na kumchania Tshirt na kumtupa nje. Bahati nzuri Q-Chilla alijulishwa kuhusu purukushani hizo, na alipoenda akasema aruhusiwe kuingia na apewe nafasi ya kuperform. Leo wale mabaunsa pengine wanatamani kuwa mabaunsa wa Diamond lakini haiwezekani.
Joseph Kabila aliwahi kuelezea kuwa kipindi anaishi Tanzania aliwahi kushushwa kwenye basi porini huko mkoani Iringa kwa sababu hakuwa na nauli ya kutosha. Alijaribu kumuomba konda amshushe angalau mahali penye mji lakini hakumuelewa. Akamtelekeza porini. Akatembea kwa mguu hadi Nyololo ndipo akapata msaada. Leo yule konda pengine anatamani kupata nafasi walau ya kumuomba msamaha Kabila lakini haiwezekani. Hakujua kama aliyemshusha porini angekuja kuwa Rais wa nchi.
Mwanzoni mwa miaka ya 1980's Meneja wa hoteli moja ya kitalii huko Hangzhou, alimnyima kazi Jack Ma. Baadaye Jack Ma alianzisha kampuni ya Alibaba na kumuajiri mtu huyo aliyemnyima kazi kuwa Meneja masoko wa online auction hosting ya Alibaba.
Maisha ni kama sarafu iliyotupwa angani, huwezi kutabiri itadondokea upande upi. Hakuna anayedumu kwenye madaraka milele. Hakuna anayekuwa tajiri milele. Hakuna anayekuwa maskini milele. Vyote hivi ni vya muda tu. Ni suala la majira na nyakati.
*Mtu unayemdhihaki leo na kumuona sawa na takataka, inawezekana ndiye atakayeamua hatma ya maisha yako kesho*. Hakuna ajuaye kesho. Mheshimu kila mtu bila kujalisha yupo katika hali gani leo kwa sababu huwezi jua kesho atakuwa wapi. Mtumishi wako wa leo anaweza kuwa boss wako wa kesho, kwa sababu kwenye maisha hakuna kinachodumu milele.
Tumia nguvu zako, utajiri wako na mamlaka yako kwa hekima ukijua kuna kesho. Siku zote simamia haki. Usimdhulumu mtu, usimnyanyase wala kumkandamiza mwenzio kwa sababu tu ya mali, nguvu au madaraka uliyonayo. Rais wa zamani wa Zimbabwe *Robert Mugabe aliwahi kusema "heshimu kila mtu kama unavyoheshimu taulo lako. Kwa sababu sehemu utakayoitumia kufutia kalio leo, kesho unaweza kuitumia kufutia uso."*
Hakuna chochote kwenye maisha yetu kinachodumu milele. Pia kumbuka hakuna tunu ya kujali wengine inayopotea bure. Jukumu la msingi la uhai tuliopewa na Mungu ni kusaidia wengine. Kwahiyo kama MUNGU amekujalia uwezo wa kifedha, au madaraka vitumie kusaidia wengine.
Na kama huwezi kuwasaidia basi usitumie cheo chako, pesa zako au madaraka yako kuwaumiza. Mahatma Ghandi aliwahi kusema kama huwezi kuwasaidia wengine basi angalau usiwaumize (If you cant help them, atleast do not hurt them).
*TAFAKARI NJEMA* mbarikiwe sana