STAA wa Bongo Fleva na bosi wa lebo kubwa ya muziki Bongo ya Konde Gang Music Worldwide, Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ au ‘Harmo’ ametangaza kulisimamisha Jiji la Dar kwa mara nyingine tena.
Harmo ameliambia IJUMAA WIKIENDA kuwa, atafanya hivyo kupitia tamasha lake kubwa linalokwenda kwa jina la Harmonize Carnival.
Kupitia Meneja wake, Beauty Mmary ‘Mjerumani’ katika mahojiano maalum na IJUMAA WIKIENDA, jamaa huyo ameahidi kufanya tamasha kubwa ambalo halijawahi kufanyika ndani ya Tanzania na hata Afrika Mashariki.
“Litakuwa ni tamasha kubwa ambalo litafanyika siku tatu likiwa na lengo la kuwa na shughuli tofautitofauti zenye kuhusiana na masuala ya kisanaa.
“Ni tamasha ambalo litatoa fursa kwa machinga, madereva na bodaboda ili kushiriki kwa namna moja au nyingine ambapo watainjoi na kufurahi kwa rika zote.
“Sidahani kama kwa Tanzania na Afrika Mashariki ilishawahi kutokea, maana tamasha litafanyika siku tatu mfululizo na litahusisha wasanii mbalimbali kutoka nje ya nchi ambao si chini ya kumi na tano. “Harmonize amekuwa ni mtu mwenye uthubutu wa kufanya vitu vya tofauti wakati wote kwa kuongeza uthamani wa kazi ya muziki ambayo tunaifanya.
“Wakati tunazindua Album ya Afro East pale Mlimani City (Dar), tulisema tutaandaa tamasha ambalo litawapa fursa mashabiki wetu na linaweza kufi ka hata mikoani na hii ni kutengeza ukaribu na mashabiki,’’ amesema Beauty Mmary.
Mwezi uliopita, Harmo aliisimamisha Dar kwa shoo ya kukata na shoka kwenye Uwanja wa Mkapa katika Tamasha la timu ya Yanga wakati wa kilele cha Wiki ya Mwananchi.
STORI: HAPPYNESS MASUNGA NA KHADIJA BAKARI, DAR