NI takriban wiki moja sasa, macho, masikio na hisia za umma zilipoelekezwa Kenya katika tukio la kaka na dada kufunga ndoa.
'Bomu' lilipasuka kilipofika kipengele cha hatua ya kuvalishana pete, mfungisha ndoa kanisani alipouliza kama kuna pingamizi lolote kama ulivyo utaratibu.
Hapo ndipo mkono wa baba mzazi uliponyooka juu, na alipopewa fursa, ‘hakupepesa macho’, akianika ukweli uliopo kwamba wote hao ni uzao wake huku umma wa cherekochereko ukibaki mdomo wazi kwa staili tofauti.
Katika ufafanuzi wake, Mzee James Sidai alibainisha kwamba, Bwana Harusi, Jonathan Munini, na Bibi Harusi, Ann Magwi, ni wa uzao wa baba mmoja ambaye ni yeye mwenyewe hata ikabidi kuzuia rasmi kufungwa kwa ndoa hiyo.
Kufuatia tukio hilo, chereko, pilau, serebuka na mengine mengi yakaishia hapo na mijadala, minong'ono, kutikisa vichwa na 'umbea', vyote vikachukua nafasi yake.
TAFSIRI PANA
Hilo lililoshuhudiwa kwa majirani Kenya huenda ni kati ya mengi yaliyochukua nafasi nchini, lakini simulizi zake hazikwenda mbali kwa sababu ya mwanya wa utandawazi na mawasiliano.
Je, nchini hali ikoje?
Nipashe ilichukua hatua ya kumdadisi Mzee wa Mila, Rocket Mwashinga, aliyekula chumvi kwa miaka 77 ambaye pia ana kofia ya pili ya wadhifa kwa kijamii akiwa Chifu Mkuu wa Mbeya Mjini na Vijijini.
Mzee Mwashinga anakiri katika jamii yake na uzoefu wa kimaisha hilo siyo jambo geni katika mazingira yake, akirejea ushuhuda wa matukio matatu, picha ileile ya kilichotokea kanisani Tana River, Kenya wiki iliyopita.
Anafafanua kuwa, walishakutana na matukio ya ndugu kupendana na kutaka kuoana na wakachukua hatua kama ya kanisani Tana River walipovunja na kupiga marufuku kimila tendo hilo.
"Kuna kijana alikaa kinyumba na mwenzake mkoani Arusha kwa muda wa miezi mitatu na alipokuwa akifanya mchakato wa mahari hapa Mbeya, alibaini binti aliyetaka kumuoa ni mtoto wa baba yake mdogo, hivyo uhusiano huo ulivunjwa kimila," anasema.
Mzee Mwashinga anaendelea: “Endapo binti angekuwa mjamzito, ingefanyika mila ya kulambishwa dawa maalum ili kukinusuru kiumbe kilichopo tumboni kisizaliwe na matatizo ya kiafya. Haiwezekani ndugu wakaoana, watazaa watoto wenye ulemavu.”
Katika kudhibiti mwelekezo huo, Chifu Mwashinga ana ushauri kwamba vijana wahakikishe kuwa kabla ya kuanza uhusiano, wachunguzane kwanza ili kujua historia ya familia zao endapo ni ndugu.
Hata hivyo, katika baadhi ya jamii nchini na hata maeneo mengine duniani, likiwamo Bara Asia, ndoa za undugu katika jozi kama: Kaka na dada; mtoto wa baba mdogo na baba mkubwa; mjomba na shangazi; ni ruksa, tena zinazoshuhudiwa na chereko za babu, bibi ndugu na jamaa.
Vilevile, yanayojiri katika mwenendo wa kiutandawazi, sasa limekuwa jambo la kawaida, vijana kuchumbiana wakiwa wamekutana katika maeneo ya mbali ndani ya nchi au nje ya mipaka ya nchi na baada ya safari ndefu huenda kukawapo mtoto au watoto na mali za pamoja kisha kunafanyika hatua ya kwenda kujitambulisha nyumbani.
WATAALAMU WA AFYA
Dk. Crispin Kahesa, ni mtaalamu bingwa anayepatikana katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) jijini Dar es Salaam, ana maoni kadhaa kwa athari zinazopatikana kwa ndoa zenye jozi ya aina hiyo.
Hivyo, Dk. Kahesa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Kinga katika taasisi hiyo, anataja njia kuu mbili za madhara ni kuendeleza vinasaba vyenye matatizo kiafya au kimwili na kurithishana magonjwa.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, magonjwa kama kisukari, selimundu, saratani, maradhi ya akili na ualbino, huendelezwa katika kizazi cha ndoa za aina hiyo tajwa.
Katika tafsiri yake ya kitaalamu, anawarejea ndugu walio wazaliwa wa tumbo moja, ndiyo hatari ya madhara ya moja kwa moja.
Shida kuu ni nini? Dk. Kahesa anafafanua: "Sababu kubwa ni vinasaba kuvurugika mpangilio wake, unakuta kinasaba kinachotengeneza chembe hai kinahama kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.
“Hatari iko wapi ndugu wakioana? Kama mmetoka kwenye familia moja, kwa kawaida vinasaba vinatokana na chembe hai mbili ambazo unaweza kukuta moja imeathirika na nyingine haijaathirika. Ili ugonjwa utokee, lazima chembe hai zote mbili zionekane na ugonjwa.
“Mara nyingi chembe hai hizi zinabebwa kwenye mayai ya mama au mbegu za baba, ili mtoto atengenezwe kuna muunganiko wa chembe hai kutoka kwa baba na kwa mama.
“Inapotokea mtu mwenye chembe hai moja yenye ugonjwa na nyingine iliyo salama na mwingine ana chembe hai moja salama na nyingine yenye ugonjwa, watu hawa wanapooana, yapo matokeo mengi yanaweza kutokea.
"Cha kwanza, zinaweza kutoka chembe hai zote salama na mtoto atakayezaliwa akawa hana ugonjwa wala hajaubeba, inapotoka chembe hai salama na ikaungana na yenye ugonjwa, usiuone ugonjwa, lakini akawa ameubeba."
Dk. Kahesa anataja uwezekano wa chembe hai za pande mbili zenye ugonjwa zikaungana na tatizo likajitokeza kwa mtoto wako moja kwa moja, hivyo familia kuwa na historia ya kuwa na magonjwa ya kurithi kama saratani, kisukari, selimundu, ualbino au ugonjwa wa akili.
Ushauri wa daktari huyo ni kwamba kunapaswa kuchukuliwa tahadhari ya kutooana ndugu ili kutoendeleza magonjwa waliyonayona pia wanajamii hao wana wajibu wa kupata ushauri wa kitaalamu na kuchukuliwa vipimo kwa mtazamo wa kudhibiti athari za kiafya.
Dk. Kahesa anasema huduma hiyo ya vipimo na ushauri kwa sasa inapatikana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) yenye maabara ya kupima vinasaba ili kugundua aina ya magonjwa ambayo familia imebeba na kupewa ushauri.
Anatoa mfano kwa ugonjwa wa selimundu, kwamba kinachopaswa kiafya ni kufunga ndoa na mtu wa jamii ya mbali ambaye pia kiafya yuko mbali na uwezekano wa maradhi hayo.
Vilevile, anasema wagonjwa wa saratani wakiwa na umri wa chini ya miaka 25, wengi wao uzoefu unaonyesha kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na kurithi.
Abainisha kuwa takwimu zinaonyesha asilimia tano ya wagonjwa wa saratani wanaangukia kwenye kundi hilo, akishauri "mtu akitaka kuoa, ni vyema aoe familia za mbali," alisema.