Kwa namna Harmonize anavyopindua hizo meza za Diamond Platnumz waweza kusema anafanya uchokozi wa makusudi, lakini ikiwa hadi anazivunja kabisa huo si uchokozi? Hapana! Hiyo ni burudani kwa mashabiki.
Kupinduliwa na kuvunjwa kwa meza hizo sio uchokozi. Vipande vya meza hizo ndio uwanja wao wa kuuza bidhaa yao kwa mashabiki. Wateja wanapenda kuona ushindani. Makala haya yanaenda kuangazia matukio machache kuhusiana na hilo.
Kofia ya Magufuli
Miongoni mwa mambo yaliyomuweka Diamond kwenye vichwa vya habari hivi karibuni ni pam-oja na kitendo cha kuvishwa kofia na Rais Magufuli wa-kati akitumbuiza kwenye kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mwanza.
Hiyo ilikuwa ni katika Uwanja wa CCM Kirumba Septemba 7 mwaka huu. Lakini Septemba 14, Harmonize akapindua meza kwenye Uwanja wa Mazaina Chato mkoani Geita.
Hii ni baada ya yeye pia kuvishwa kofia na mgombea Urais Magufuli kama ilivyotokea kwa Diamond na ni aina ile ile ya kofia. Kama ni mchezo wa soka, basi hapo ubao wa matangazo ungesoma goli 1-1, lakini kwa kawaida siku zote anayesawazisha ndiye mwenye furaha zaidi.
Simba na Yanga
Agosti 22 mwaka huu Diamond alibeba vichwa vya habari vya wasanii waliotumbuiza katika kilele cha Tamasha la Simba Day kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam. Diamond alishuka uwanjani kwa helikopta uwanjani hapo na kutoa burudani ya nguvu.
Siku chache mbele wapinzani wa jadi wa Simba SC, Yanga SC wakamtangaza Harmonize kuwa atatumbuiza kwenye Kilele cha Wiki ya Mwananchi, Agosti 30. Ndipo Harmonize akaanza mikakati ya kupindua meza za Diamond na kuzivunja kibabe.
Kwanza alifika Uwanja wa Mkapa siku moja kabla ya shughuli yenyewe na kufanya majaribio ya sauti (soundcheck), alitua uwanjani kwa kutumia helkopta. Pili akatoa wimbo maalumu wa Yanga kwa ajili ya siku hiyo kama alivyofanya Diamond kwa Simba.
Siku ya tukio lenyewe akaingia uwanjani kwa kushuka kwa kamba kwanza akitambaa nayo juu kama maninja au wanajeshi wanavyovuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine na kile kilichoelezwa kuwa alianguka ndicho kilichompatia ushindi. Aligonga vichwa vya habari kuliko, ukizingatia tamasha hilo la Yanga lilijaza watu wengi zaidi ya lile la Simba alilotumbuiza Diamond.
Lebo
Mara baada ya kuondoka WCB ya Diamond, Harmonize aliamua kuanzisha lebo yake, Konde Music Worldwide maarufu Konde Gang na kuanza kusimamia wasanii. Katika upande wa lebo Harmonize amefanikiwa kujibu mapigo ya Diamond mara tatu.
Kwanza; ni pale usiku wa Aprili 8 mwaka huu Diamond alipotangaza kumsaini Zuchu ndani ya WCB. Siku tatu mbele, yaani Aprili 11 mwaka huu tena usiku, naye Harmonize akatangaza kumsaini Ibraah katika lebo yake ya Konde Music.
Pili; hadi kufikia sasa sasa chini ya WCB Diamond anasimamia wasanii watano ambao ni Rayvanny, Queen Darleen, Lava Lava, Mbosso na Zuchu. Idadi hiyo ni sawa na ile ya Harmonize ndani ya Konde Music yenye wasanii Ibraah, Country Boy, Cheed, Killy na Skales.
Tatu: Julai 19 mwaka Diamond alimzawadia msanii wake mpya Zuchu gari, ilipofika Septemba 11 naye Harmonize akatoa magari mawili kwa mpigo kwa wasanii wake wapya, Ibraah na Country Boy.
Albamu
Machi 14, 2018 Diamond alizindua albamu yake ‘A Boy From Tandale’ Nairobi nchini Kenya, ilipofika Machi 14, 2020 naye Harmonize akazindua Albamu yake ‘Afro East’ Mlimani City Dar es Salaam. Hapo ukitazama ndio utajua Konde Boy kadhamiria kweli kupindua meza za Simba, kivipi?
Mosi; Tarehe ya kutolewa kwa albamu hizo zimefanana, kilichopishana hapo ni miaka tu, yaani ya Diamond ilitoka 2018, ya Harmonize 2020, huku zote zikiwa na nyimbo 18.
Pili; A Boy From Tandale ya Diamond imemshirikisha msanii mmoja pekee wa kike kutokea Tanzania ambaye ni Vanessa Mdee aliyesikika kwenye wimbo uitwao Far Away. Huku Afro East ya Harmonize ikimshirikisha msanii mmoja pekee wa kike kutokea Tanzania ambaye ni Lady Jaydee aliyesikika kwenye wimbo uitwao Wife.
Tatu; Kwa ujumla Albamu zote mbili zina watu watatu watatu walioshirikishwa kwenye nyimbo kutokea Tanzania. Ndiyo!, A Boy From Tandale ina Vanessa Mdee, Rayvanny na Young Killer, huku Afro East ina Lady Jaydee, Mr. Blue na DJ Seven.