Kufuatia kukamatwa kwa mipira ya kiume (kondomu), 345,000 ambazo zimekwishatumika na kusafishwa kisha kurudishwa madukani baadhi ya wananchi wa Vietnam wamesema kuwa bidhaa hizo zisiuzwe kwa rejareja badala yake ziuzwe katika maduka maalumu ambayo yamethibitishwa na shirika la afya.
Jeshi la polisi la nchini Vietnam lilikamata mipira hiyo ya kiume 345,000 zilizotumiwa ambazo ziliripotiwa kumwagiwa maji ya moto kwa ajili ya kusafishwa ili kurejeshwa tena sokoni.
Mipira hiyo ya kiume ambayo ni zaidi ya kilo 360 zimekamatwa katika jiji la Ho Chi huko Vietnam baada ya mkazi aliyekuwa jirani na eneo la tukio kutoa taarifa ambazo zilichunguzwa na jeshi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kituo cha serikali cha Vietnam Televisheni (VTV) ilionyesha mifuko mikubwa iliyo na dawa zinazotumiwa kwa ajili ya zoezi hilo.
Mwanamke aliyekamatwa baada ya polisi kuvamia eneo hilo ameeleza kuwa wamekuwa wakizichemsha kisha kuzianika katika mti na kuandaliwa kwaajili ya kuuzwa tena.
Lakini mpaka sasa jeshi la polisi halijatoa tamko rasmi kuhusiana na tukio hilo kutokana na kufuata taratibu za kisheria