WANAFUNZI wawili wa Shule ya Msingi ya St Claret ya jijini Dar es Salaam, wamekufa baada ya kudaiwa kuzama kwenye bwawa la kuogelea jirani na shule hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Edward Bukombe alisema jana kuwa Polisi wana taarifa kuhusu vifo vya wanafunzi hao wa Shule ya St Claret iliyopo Kimara Kingóngó (Michungwani).
“Ni kweli tuna taarifa za watoto wawili kufa wakati wakiogelea, inadaiwa awali waliogelea wakamaliza, halafu inaelekea wakashauriana tena warudi kuogelea, ndipo wakaenda kwenye kina kirefu wakazidiwa maji na kufa,”alisema Kamanda Bukombe.
Alisema Polisi wamewakamata wamiliki wa bwawa hilo, lililojengwa kwa ajili ya biashara na wanaendelea kuchunguza undani wa vifo hivyo.
“Tunawashikilia wamiliki, bwawa la kuogelea lazima kuwe na mtu anayejua kuogelea yaani msimamizi na anakuwepo hapo wakati wote wa huduma, sasa hawa watoto inaonekana walizidwa maji, walienda kwenye kina kirefu, na hawakupata msaada, hadi umauti,”alisema Kamanda Bukombe.
Alisema taarifa zaidi kuhusu tukio hilo la juzi zitatolewa leo.
Awali, mashuhuda walidai kuwa mmoja watoto hao anadaiwa kuwa wa darasa la tatu na mwingine la sita, na kwamba walidanganya nyumbani kwao kuwa walikuwa wanakwenda kwenye mahafali shuleni hapo, jambo ambalo si kweli.
Ilidaiwa na mashuhuda kuwa, kulikuwa na mahafali ya darasa la saba shuleni, lakini wanafunzi waliokufa hawakwenda kwenye sherehe kama walivyoaga nyumbani, ila walikwenda kuogolea.
Hadi jana jioni taarifa kutoka shuleni hapo zilidai kuwa uongozi wa shule uliitisha kikao cha dharura kujadili jambo hilo, kwa kuwa vifo vya watoto hao viligundulika baada ya wazazi kuona usiku ukiingia bila watoto wao kurudi ndipo waliuliza shuleni. Shuleni hawakuwepo ndipo juhudi za kuwatafuta zilianza na ikafahamika kuwa miili ilikuwa imehifadhiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila.