UONGOZI wa Klabu ya Yanga umesema mpaka sasa bado haujajibiwa barua yao na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) juu ya kesi yao na kiungo mshambuliaji wa Simba, Bernard Morrison.
Yanga ilipeleka malalamiko yao Fifa kupinga maamuzi ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji hivi karibuni baada ya kutoa hukumu ya Morrison kuwa mali ya Simba jambo ambalo hawakuridhika nalo.
Yanga inadaiwa kuwa ilimpa mkataba wa miaka miwili Morrison lakini sakata hilo lilipopelekwa kwenye kamati hiyo ilibaini upungufu kadhaa kisha kudai ni mchezaji huru, hivyo akatua Simba na tayari ameanza kuitumikia kwenye mechi za ligi.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema, bado wanaendelea kusubiria majibu yao kutoka Fifa ambapo hawajui lini watayapata.
“Suala la Morrison hadi sasa bado hatujalipatia majibu kwa kuwa tunasubiria majibu kutoka Fifa na watakapotupatia ndiyo tutatoa taarifa ila kwa sasa hatujui lini watatujibu, lakini hakuna kilichotukwamisha,” alisema Mwakalebela