JPM: Kumbe Zitto Naye Anapanda Ndege Zetu!



MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho, John Magufuli, ameshangazwa na kitendo cha aliyekuwa mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe kutumia ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) zilizonunuliwa na serikali licha ya kuziponda na kupinga maendeleo hayo ya ndege.

Magufuli amesema hayo leo, Septemba 18, 2020, wakati akiwahutubia wananchi wa Kigoma katika kampeni zake alizofanya kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma Mjini.

“Nilikuwa naonyeshwa hapa picha Mheshimiwa Zitto akishuka kwenye ndege tulizonunua, nikafurahi sana nikasema kumbe hata wanaopinga ndege zetu, nao wanazipanda? Lakini kwa nini na nyie watu wa Kigoma mlisubiri kuja kunionyesha mimi, si mngemuonyesha tu yeye? Maendeleo hayana chama.
“Ujenzi wa barabara za lami, mifereji ya maji pamoja na uwekaji wa taa hapa Kigoma mjini ulitekelezwa ndani ya ilani ya CCM na mimi ndiyo msimamizi wake na ninafahamu hela zilitoka wapi.
“Wale waliotamani sisi tufe wameshindwa na leo wanapata aibu kubwa, ninaomba muwape hizo salamu kwamba hatufi na wala hayupo wa kufa kwa sababu Mungu anawapenda wana Kigoma na Watanzania.
“Tena nakumbuka wapo na nyinyi wengi mnawafahamu walizungumza kwamba, sisi tunajidai kumwamini Mungu na kudharau masuala ya sayansi tujiandae watu wapatao zaidi ya milioni nne watafariki kutokana na Corona hapa Tanzania, leo wanaona aibu.
“Hatukutaka kufungiwa ndani hata kuku wanaofugwa na kufungiwa ndani wanapata mateso, watu walikuwa wamejiandaa kuoa na wengine kuolewa, ukifungiwa utampata wapi binti mzuri atakayekutunza katika maisha yako?
“Ninaomba radhi kwa wana Kigoma wote walionisubiri njiani na walipenda sana niongee nao kwenye vituo mbalimbali, lakini sikuweza kusimama na kuongea na nyinyi kwa kuzingatia sheria za uchaguzi, mwisho wa kampeni ni saa 12 jioni, siwezi kuvunja sheria,” ni baadhi ya kauli alizotoa Magufuli.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad