MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli amemtaka mgombea wa kiti hicho kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kuachana na kinyang’anyiro hicho kwani hatoshinda, na badala yake asubiri (Magufuli) akishinda ampe kazi yoyote serikalini.
Magufuli amesema hayo leo Jumanne, Agosti 1, 2020 wakati akizungumza na wananchi wa Ikungi, mkoani Singida kwenye kampeni zake akiwa njiani kuelekea Singida Mjini ambako atafanya mkutano mkubwa leo hii hii.
“Katika miaka inayokuja mtaona treni ya umeme inayokimbia kilomita 160 kwa saa, leo nikizungumza mtaona kama ni miujiza, lakini tunataka tuitengeneze Tanzania iwe kama Ulaya. Ndiyo maana nasikitika wasiponichagua nani atakuja kuyajenge haya?
“Wengine wanaweza wakaja wakabomoa hata haya mataaluma. Tunajenga umeme Mradi wa Nyerere unagharimu trilioni 6.5, mradi ukikamilisha bei ya umeme tutashusha, bahati nzuri miradi yangu inapitishwa na wabunge wa CCM, wabunge wa vyama vingine huwa wanatoka bungeni, nani atapitisha hiyo bajeti?
“Miradi ya halmashauri kuna pesa ambazo huwa tunatoa, nani atasimamia hiyo miradi, lazima asimamie mtu ambaye akishindwa nitamtumbua hukohuko, ukililetea wa chama kingine nitashindwa, ndiyo maana naomba mniletee hawa madiwani wa CCM.
“Ninajua mmoja wa wagombea nafikiri anatoka hapa (Ikungi – Singida) mshaurini kwamba mimi mnipe kura nyingi halafu yeye nitamtafutia kikazi kidogokidogo serikalini, ni mtoto wetu tunampenda, wala hatuna tatizo na mimi sina tatizo na mtu yeyote, kwani kazi lazima uwe rais?
“Urais muachie Magufuli na wewe tutakupa kikazi kidogodogo ambacho utaweza kufanya, akija mwambieni Magufuli amesema atakupa kazi, kwa nini unahangaikia hii kazi ambayo hautashinda?” amesema Magufuli bila kumtaja mtu kwa jina.