Kansa ya Macho Yamtesa Mtoto wa Mwaka Mmoja



Hujafa hujaumbika! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mtoto Rehema Baraka, mwenye umri wa miezi (11) mkazi wa Kibaha mkoani Pwani, kuzaliwa na tatizo la kansa ya macho, ambalo limesababisha kupata upofu na kuwa kiziwi

Akizungumza kwa simanzi na UWAZI, mama mzazi wa mtoto huyo, Nadya Faustine (23), amesema tatizo la mtoto wake lilianza baada ya kupata ujauzito wa watoto mapacha, ambao mmoja wao alifariki akiwa tumboni.


 


“Mwanzo niligundulika kuwa na ujauzito wa watoto mapacha, ulipofikisha miezi minne, mtoto mmoja alifariki akiwa tumboni.


 


“Hospitali nikashauriwa nisubiri hadi miezi 6 ili mtoto mzima aweze kukua, nikasubiri mpaka ilipofika miezi 6, nikaenda hospitali kujifungua na nikafanikiwa kujifungua kwa upasuaji, ambapo yule mtoto aliyefariki alitolewa akiwa ameharibika.


 


“Hali hiyo ilisababisha matatizo kwa huyu mwanangu mzima kwa sababu alizaliwa akiwa ameambukizwa kansa ya macho na hana uwezo wa kuona pamoja na ulemavu wa kusikia (Kiziwi),’’ alieleza Nadya.


 


Alisema kutokana na matatizo hayo, anaomba msaada kwa wasamaria wema ili kutibu tatizo la mtoto wake. “Kwa sasa nawaomba sana wasamaria wema wanisaidie ili mwanangu aweze kutolewa haya macho, kwani yakiendelea kubaki, kansa itasambaa hadi kwenye ubongo,’’ alisema Nadya.


 


Aidha, Mama wa mtoto huyo akaendelea kwa kusema, kwa sasa hana mahali pa kuishi, kwani yeye ni mwenyeji wa Mwanza, lakini alienda Kibaha mkoani Pwani, kufanya kazi za ndani.


 


“Sina mahali pa kuishi, nilienda Kibaha kwa ajili ya kufanya kazi za ndani, lakini kutokana na matatizo niliyoyapata, nikafukuzwa.


 


“Mimi ni mtoto pekee kwenye familia yangu, baba yangu ameshafariki dunia miaka mingi iliyopita, nimebaki na mama ambaye naye sina mawasiliano naye mazuri kutokana na kubeba ujauzito, jambo ambalo limemuumiza na kupelekea kunikataa kama mtoto wake,’’ alimalizia Nadya.


 


Naye jirani wa Nadya, aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma, aliwaomba Watanzania wamsaidie Nadya, kwani anapitia wakati mgumu.


 


“Nadya anahitaji msaada, kwani anapitia wakati mgumu kwenye umri mdogo, ukiangalia mama yake mzazi amemkana na hakuna mwingine anayemtegemea. Tunaomba wasamaria wamsaidie,’’ alisema Fatuma.

Kwa aliyeguswa na mkasa wa binti huyu, unaweza kumsaidia kupitia namba 0678 641 038 jina Nadya Faustine.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad