JANA na leo kumezuka mijadala huko kwenye mtandao wa Twitter, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Nzega Vijijini, Khamis Kigwangala ameuamsha upya mjadala wa Bilioni 20 za Mo Dewji kwa Simba.
Iko hivi miaka mitatu nyuma wakati Klabu ya Simba ikiingia kwenye mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji pia ilisaini makubaliano ya umiliki wa hisa kati yao na mwekezaji, Bilionea Mohammed Dewji.
Makubaliano yao ilikua ni Simba kumiliki hisa asilimia 51 na Mo Dewji kumiliki asilimia 49 huku akiingia Klabu kiasi cha fedha za kitanzania Sh Bilioni 20 kama sehemu ya dili hilo.
Sasa Kigwangala ameibuka na kusema Mo Dewji hajalipa hizo Bilioni 20 na kwamba anataka mwekezaji huyo aeleze lini anaziweka fedha hizo au kama vipi 'asepe'.
Na hii imekuja baada ya Simba kumtangaza mwanadada Barbara Gonzalez kuwa CEO mpya wa Timu hiyo.
Mimi sitotaka kujadili 'personality' zao kama ambavyo wao wameanza kushambuliana huko twitter ila ningependa tujadili mambo ambayo Mo kayafanya Simba ndani ya miaka mitatu aliyokuepo kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Mwekezaji wa Klabu.
Tukumbuke kabla ya ujio wa Mo, Simba ilikua haijachukua ubingwa wa Ligi Kuu nchini kwa misimu minne mfulululizo. Kombe lilienda Azam kisha Yanga wakabeba mara tatu mfululizo.
Siyo kwamba Simba haikuepo, ilikuepo ila haikua na uwezo wa kushindana na Yanga na Azam kuanzia ndani ya uwanja hadi nje ya uwanja.
Simba ilikua haitishi tena, ilisajili wachezaji wa kawaida kutoka nje ya Nchi kwa sababu hata pesa hawakua nayo, ilisajili wachezaji wa kawaida kabisa. Ushindi ungetoka wapi wakati straika unaemtegemea ni Papa Ndaw ambaye kiatu chake tu kimechanika?
Simba haikua na uwanja wa mazoezi, walitegemea viwanja vya kukodi sana sana ungewakuta Uwanja wa Kinesi.
Eneo lao kule Bunju liligeuka kuwa pori ambalo pengine fisi na wanyama wengine walikuepo kwa sababu ni kama kulishatekelezwa.
Miaka mitatu ya Mo ndani ya Simba tumeshuhudia mabadiliko ambayo yameiletea Klabu mafanikio makubwa na ya haraka kulinganisha na kipindi cha nyuma.
Tunavyozungumza leo Simba ina viwanja viwilo vya kisasa vya mazoezi Bunju, Timu sasa inaepukana na gharama za kukodisha viwanja kwa ajili ya mazoezi.
Miaka mitatu ya Mo, Simba imeshinda matatu ya Ligi Kuu tena mfululizo na kuweka rekodi yao kama klabu, imetwaa mataji mawili ya kombe la shirikisho 'FA', imetwaa makombe manne ya ngao ya Jamii.
Baada ya kitambo kirefu cha kutaniwa na wenzao wa Yanga kwamba ni wa matopeni kwa sababu haichezi michuano ya Kimataifa hatimaye Simba imeshiriki mashindano ya kimataifa.
Siyo tu imepanda ndege kucheza kimataifa lakini pia msimu wa mwaka 2018/19 ilifuzu hatua ya Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika na kuweka rekodi ya Nchi.
Mafanikio yote haya yametokana na nguvu ya Mo katika kuwekeza kwenye usajili, benchi la ufundi, kugharamia kambi na kuweka mazingira mazuri kwa Timu katika kufanya vizuri.
Ndani ya miaka mitatu ya Mo, Simba imewekeza kwenye Soka la Vijana na Soka la Wanawake, msimu huu tumeshuhudia timu zote tatu za Simba zikichukua makombe ya Ligi.
Sasa tunapoona mashabiki wa Simba wakianza kuleta chokochoko ndani ya klabu maana yake wameshiba na wanataka kurudi kule kule walipokua.
Hawa wanaompinga Mo Dewji kipindi hayupo hatukuwahi kujua kama ni mashabiki wa Simba, hawakuwahi kutoa mchango wao wowote kwa Klabu.
Zaidi ya Sh Bilioni 4 zinatumika kila mwaka kugharamia mahitaji ya Klabu, fedha zote hizo zinapatikana kutokana na uwekezaji wa Mo Dewji, hawa wanaopinga uwekezaji wake leo wanaweza kusaidia usajili wa Benard Morrison au Clatous Chama?
Tujikite katika kuangalia namna gani tutaboresha akademi za Soka kwa ajili maendeleo ya vijana na soka la wanawake. Tuache kushambulia watu wanaotumia akili na gharama zao kukuza timu zetu.
Yanga wamepita kwenye msoto mkali kwa misimu minne baada ya kumtibua Yusuf Manji, leo wamewapata GSM wanawakumbatia maana wanajua maumivu waliyopitia miaka minne hadi kufikia kupitisha bakuli la michango.
Leo tunashabikia Manchester United bila hata kujua Familia ya Glazer ambao ni wamiliki wanapata faida gani kuwekeza United, wanachoangalia mashabiki no furaha ya kupata matokeo na kuchukua makombe.
Swali lingine la kujiuliza anayeshambulia kueleza kuhusu Bilioni 20 ni Dewji lakini watu hawawaulizi viongozi wa Simba akina Mwina Kaduguda, tafsiri yake hapa kinachotafutwa siyo Bilioni 20 bali ni Mo Dewji.