Kisa cha Mwalimu Aliyekutwa 'Guest' na Mtoto




TAKUKURU mkoa wa Mbeya, inamshikilia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyeregete iliyoko wilayani Mbarali, Adelhard Mjingo, (44), kwa tuhuma za kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 14 kwa ahadi ya kuwa angemsaidia kufaulu mitihani.

Taarifa hiyo imetolewa leo Septemba 25, 2020 na mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Mbeya Julieth Matechi, na kusema kuwa mwalimu huyo alinaswa na makachero wa TAKUKURU mnamo Septemba 23 mwaka huu akiwa na mwanafunzi huyo kwenye moja ya nyumba za kulala wageni.

Matechi amesema, siku ya tukio mwalimu huyo aliaga shuleni kuwa anaenda kwenye semina ya chanjo katika Mji wa Rujewa wilayani humo na aliondoka pamoja na walimu wenzake lakini alipofika kwenye ukumbi aliandikisha jina na kuomba udhuru kisha akaondoka na kwamba wakati mwalimu huyo anaondoka shuleni alimtaka mwanafunzi wake aende nyumbani kubadili nguo.


"Mwalimu huyo alichukua chumba kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Executive iliyopo Rujewa na kisha akamtuma dereva bodaboda kwenda kumchukua binti huyo na alipofika naye mwalimu alimpokea na kuingia naye chumbani, baada ya kuingia na mwanafunzi huyo chumbani alitoka na kwenda kumnunulia chipsi na soda kisha akaingia tena chumbani kwa ajili ya kutimiza azma yake", amesema mkuu wa TAKUKURU.


Aidha Matechi ameongeza kuwa wakati mwalimu huyo akijiandaa kutekeleza uhalifu huo, makachero wa TAKUKURU waliokuwa wanafuatilia tukio hilo waliingia na kumuweka chini ya ulinzi mwalimu huyo, na kwa sasa taasisi hiyo inaendelea na uchunguzi na utakapokamilika atachukuliwa hatua za kisheria.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad