Kisa Corona Msuva Ashuka Thamani



THAMANI ya mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva anayeichezea Difaa El Jadida ya Morocco kwa sasa imeonekana kushuka kutoka Sh.2.4 bilioni hadi Sh.1.5 bilioni kwa mujibu wa mtandao wa Transfermarkt.


Msuva ambaye amekuwa akihusishwa na klabu ya Ligi Daraja la Kwanza nchini Ufaransa ‘Ligue 2’, iitwayo Le Havre anashika nafasi ya pili nyuma ya Samatta kati ya wachezaji wa Kitanzania wenye thamani kubwa zaidi.



 

Samatta anaongoza orodha hiyo akiwa na thamani ya Sh. 25 bilioni huku kwa mujibu wa mtandao huo, akioneka kushuka kwa Sh.7 bilioni tangu alipojiunga na Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu England.


Nyota huyo wa zamani wa Yanga, ameonekana kutokuwa kwenye kiwango bora msimu huu kama ilivyokuwa katika msimu miwili iliyopita ambapo alikuwa miongoni mwa washambuliaji ambao walikuwa wakiwania kiatu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu nchini Morocco.


Hadi sasa ambapo imesaliwa michezo minne kabla ya msimu huu kumalizika ambayo ni dhidi ya Hassania Agadir, Rapide Oued Zem, FUS Rabat na Youssoufia Berrechid, Msuva amefunga mabao matano tu kwenye michezo 25 ya Batola Pro.


Msimu wake wa kwanza Morocco ambao ulikuwa wa 2017/18, Msuva alimaliza Ligi akiwa na mabao 11 huku msimu uliofuata akivunja rekodi yake ya msimu wake wa kwanza kwa kupachika mabao 13.


Kwa wastani wa mabao ambayo amekuwa akifunga msimu huu, ni ngumu kwa Msuva kufikia idadi ya mabao ambayo aliifungia Difaa El Jadida kwa misimu miwili iliyopita.


MSIKIE MSUVA


Kusimama kwa Ligi Kuu Morocco kutokana na janga la corona, Msuva anaamini imechangia kwa wachezaji wangi kurudi nyuma. “Ninachoomba Mungu ni kuona namaliza msimu salama kwa sababu umekuwa na changamoto nyingi.


“Kusimama kwa ligi na kurejea ni kama ndo tulikuwa tunaanza upya msimu mwingine, hatukuwa bora tulivyorejea,” alisema mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania.


Kuhusu uwezekano wa kuondoka baada ya msimu kumalizika, Msuva alisema hilo ni jambo la kusubiri na kuona nini kitatokea.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad