Na Bwanku M Bwanku
Biashara ni moja ya sekta kiini na kichocheo kikubwa sana cha maendeleo ya viwanda na sekta nyingine zinazogusa maisha ya watu kiuchumi na kijamii. *Sura ya Pili ya Ilani ya CCM* iliyoeleza *mapinduzi ya uchumi kwa maendeleo kwa watu* imefafanua kwa upana mafanikio makubwa yaliyopatikakana kwenye sekta hii na kuweka mipango na mikakati mingine mikubwa ya kuboresha na kuimarisha sekta hii kwa miaka mitano ijayo.
*Kipengele cha 47 cha Ilani ya CCM kilichoanzia ukurasa wa 59 hadi 60* kimeeleza mafanikio lukuki yaliyopatikana kwenye miaka mitano iliyopita ambayo yamewekewa mikakati zaidi ya kuboreshwa na kuimarishwa zaidi kwa miaka mitano ijayo. Mafanikio hayo ni pamoja na:-
Kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa na huduma kwenye masoko ya kikanda (preferential market access) ambapo kwa upande wa Jumuia ya Afrika Mashariki kutoka mwaka 2015 hadi 2018 Tanzania imekuwa urari chanya wa mauzo ya bidhaa kwa wastani wa Dola za Kimarekani milioni 288.04 ambapo bidhaa za madini ya Tanzanite, Chai, Kahawa, Sigara, Dawa na Vifaa Tiba, Kuimarisha mahusiano ya kibiashara za nje ikiwemo nchi za Ulaya na Asia kama Uswisi na India ambapo mauzo ya Tanzania yaliongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 153.93 mwaka 2015 hadi 257.17 kule Uswisi na kutoka Dola za Kimarekani milioni 20.55 mwaka 2015 hadi milioni 42.42 kule India.
Zaidi Serikali iliendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini kwa kuandaa na kutekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini *(Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment)* ambao ulifuta tozo kero 168 ambazo kati yake 114 zikiwa kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Vilevile tozo 54 za TBS, OSHA na iliyokuwa TFDA nazo zilifutwa hali ambayo imechochea urasimishaji wa biashara mbalimbali.
Serikali ilianzisha kutumia soko la bidhaa na kupunguza upotevu wa mazao baada ya uzalishaji ikiwemo na kujenga maghala katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Maghala kule Mvumi Scheme, Kilosa, Msola Ujamaa Scheme, Njage Scheme, Mbogo Komtonga na Kigugu, kuongeza kwa uwazi na ushindani sanjari na kuimarisha bei za mazao na kuwanufaisha wakulima kwa kushirikisha wadau mbalimbali ikiwemo vyama vya ushirika.
Kuongeza wigo wa biashara kati ya Tanzania na nchi jirani ambapo vituo 8 vya kibiashara vya Holili/Taveta, Sirari/Isebania, Namanga/Namanga, Kabanga/Kabero, Rusumo, Mtukula, Horohoro/Lungalunga na Kituo cha Tunduma/Nakonde vilianzishwa. Zaidi Serikali ilirahisisha utaratibu wa usajili na utoaji leseni kwa kuanzisha mfumo wa usajili wa majina ya biashara, makampuni, alama za biashara na huduma, leseni za viwanda kwa njia ya mtandao tu kupitia anuani ya Brela yaani www.brela go.tz.
*Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 hadi 2025 katika kipengele cha 49* katika kuimarisha sekta hii muhimu kimapato ndani na nje, Serikali itakayoundwa na CCM itaendelea kuhakikisha mchango wa sekta ya biashara kwenye Pato la Taifa unaendelea kuimarika zaidi kwa kutekeleza kwa vitendo yafuatayo:-
(a) *Kuweka mazingira wezeshi ya biashara na kuhakikisha kwamba zinapatikana fursa nafuu za biashara ili kuchochea ujenzi wa viwanda na uzalishaji wa bidhaa zenye ubora wa kimataifa na zinazohimili ushindani.*
(b) *Kubuni na kutekeleza mikakati ya kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini kwa kuimarisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini yaani Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment ikiwa pamoja na kudhibiti utoaji wa leseni, kupunguza idadi na viwango vya tozo, ada na kodi zisizofaa.*
(c) *Kuratibu na kujenga masoko ya kimkakati katika maeneo ya mipakani ili kuwapa wakulima, wajasiriamali wadogo hususan wanawake na vijana fursa ya kuuza mazao yao nje ya nchi. Pia kuwaunganisha wafanyabiashara na wasindikaji kwenye masoko ya ndani na nje kupitia mfumo maalum.*
(d) *Kubuni na kutekeleza mikakati ya kutoa elimu na kuondoa vikwazo vya utaratibu wa stakabadhi ya mazao ghalani ikiwa ni pamoja na kuhamasisha sekta binafsi kujenga miundombinu ya maghala bora ya kuhifadhia mazao mbalimbali hususan vijijini.*
(e) *Kufanya mapitio na maboresho ya sera na mikakati mbalimbali itakayoimarisha mazingira ya ufanyaji biashara na kukuza biashara ndani na nje ya nchi.*
*TUMETEKELEZA KWA KISHINDO, TUNASONGA MBELE PAMOJA.*