Kitendo cha rais Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ kumpa staa wa muziki barani afrika, Nasibu abdul ‘Diamond Platnumz’ kofia yake, ilikuwa ni zaidi ya heshima, lakini ukienda mbali zaidi, kuna jambo kubwa zaidi ambalo linakwenda kumuongezea mamilioni, IJUMaa linakupa mchongo kamili!
TUJIUNGE NA CHANZO
Taarifa za ndani kutoka kwenye lebo ya staa huyo ya Wasafi Classic Baby (WCB) zinaeleza kuwa, tukio hilo wamelichukulia kwa uzito mkubwa na limeandika historia nyingine kwenye maisha ya Diamond au Mondi.“Tumelipa uzito mkubwa sana, kitendo cha Rais kuvua kofia yake na kumpa mtu, siyo jambo dogo. Ni jambo la kihistoria.
Kumbukumbu zangu zinaniambia kwamba, haijawahi kutokea,” kilisema chanzo hicho.Kikizidi kufunguka kuhusu heshima ya kofia hiyo, chanzo hicho kilisema mbali na kuhifadhi kwenye sehemu maalum ya kutunzia tuzo za Mondi, wanafikiria kuandaa shoo moja kubwa ya kuonesha mashabiki jinsi gani wameheshimishwa na kiongozi huyo mkuu wa nchi.“Tunafikiria kuandaa hata shoo moja kubwa sana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, baada ya mheshimiwa Magufuli kuchaguliwa tena kwa mara nyingine Oktoba 28, mwaka huu.
NI SHOO YA USHINDI…
“Itakuwa ni kama shoo ya ushindi kwa Rais wetu, lakini pia shoo ya kurudisha heshima kwa mashabiki wetu, ambao ndiyo chachu ya sisi kufanya vizuri hivi hadi kufikia hatua ya Rais wetu kututunuku kofia ile,” kilisema chanzo hicho
KUINGIZA MILIONI 600
Chanzo hicho kilieleza kuwa, mpango wa shoo hiyo ambao ndiyo wanaendelea kuuchakata, unaonesha kuwa wanatarajia kuingiza zaidi ya shilingi milioni 600.“Si unaju balaa la Mondi? Sasa akiwa na Wasafi wote itakuwaje? Hakuna shaka kwamba tunaujaza ule uwanja kwa kiingilio cha shilingi elfu kumi tu. “Sasa piga mahesabu elfu kumi mara watu elfu sitini wanaoingia Taifa na hapo bado kuna wengine wa V.I.P ambao wataingia kwa kiingilio kikubwa zaidi,” kilisema chanzo hicho huku kikibainisha kuwa, sehemu ya pesa hizo watazipeleka kwa watu wanaoishi kwenye mazingira magumu.
MENEJA AFUNGUKA
Gazeti la IJUMAA lilimvutia waya mmoja wa mameneja wa Mondi, Said Fella ‘Mkubwa Fella’ ambapo kwa upande wake hakutaka kueleza kuhusu mkakati huo wa shoo, lakini zaidi alisema kuwa wao kama viongozi, wamefurahishwa na suala la Rais kumpa kofia Mondi.
“Sisi kama viongozi wa Nasibu (Mondi), tunachukulia hili kama ni kitu kikubwa sana, tunaona ile zawadi imetoka kwa Mungu, Mheshimiwa Rais amepewa uwezo na Mungu kamzawadia kijana wetu kuonesha kwamba, Mondi naye ana thamani katika Taifa letu.
“Lakini mbali na hapo, tumeona ni kitu kikubwa sana kwa sababu kitu chochote cha Rais kumpa raia wa kawaida kitu kama kile, ni kitu kikubwa sana na ndiyo maana na yeye Mondi ameiweka ile kofia kama ni tuzo kwenye kabati lake ili iwe kumbukumbu kwa wajukuu zake, kwamba kuna kitu alikifanya duniani na akapata heshima kama hiyo, kilichobaki ni kuhakikisha tunaendelea kumsapoti Rais wetu ili apate kura nyingi zaidi,” alisema Fella ambaye ni mgombea wa nafasi ya Udiwani wa Kata ya Kilungule wilayani Temeke, Dar.
TUJIKUMBUSHE
Mondi alipewa zawadi hiyo ya kofia alipokuwa kwenye kampeni za CCM katika Uwanja wa CCM-Kirumba jijini Mwanza, ambapo mbali na yeye, wasanii wengine walipata wasaa wa kupafomu.
Awali, walianza kupafomu wasanii wengine ndipo baadaye Mondi naye akapewa nafasi na baada ya kumaliza kupafomu, msanii huyo aliaga mashabiki wake ndipo Rais Magufuli alipomuita na kumtaka apande meza kuu alipokuwa ameketi yeye na viongozi wengine.Mondi alipanda kwenye meza kuu ambapo Rais aliichukua kofia hiyo yenye jina lake na kisha kumvalisha Mondi.