MGOMBEA wa Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli amewambia wapiga kura wake kuwa anasiri kubwa na nzito ndani ya moyo wake juu ya jiji la Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine ameutaja uamuzi wake wa kuhamia Dodoma kuwa ni kutokana na upendo mkubwa alionao kwa watani zake Wagogo.
Mapema leo Septemba, 28, akiwahutubia wakazi wa Chipogolo (Dodoma) mgombea huyo wa CCM alisema kuwa anatamani kuona jiji la Dodoma linazidi kustawi maradufu zaidi ya jiji lolote nchini, huku akitaja miundo mbinu mbalimbali ambayo inajengwa katika jiji hilo kama kichocheo cha kulikuza jiji hilo dhidi ya majiji mengine.
“Tunataka Dodoma tuibadilishe hiyo ndiyo siri iliyomo moyoni mwangu, nataka Dodoma ndilo liwe jiji kubwa kuliko majiji yote katika nchi ya Tanzania, tumejipanga vizuri mno na ndiyo maana hata ring road ya kilometa 110 yenye njia nne tunaanza kuzijenga huku” amesema Dkt John Magufuli.
Aidha Magufuli amelitaja jiji la Dodoma kama mkoa ambao ulipigwa vita sana kwa kile alichokitaja kuwa baadhi ya watu waliona kuwa mkoa huo haukustahili maendeleo ambayo yamekuwa yakipelekwa katika jiji hilo, jambo ambalo anasema kwa upande wake hakubaliani nalo.
“Dodoma ilipigwa vita mno kwamba hapafai kuwa makao makuu, Dodoma palipigwa vita mno kwamba hawafai haya maendeleo mnayotakiwa kuyapata, nimeamua kwamba mimi naenda kukaa Dodoma, shukrani pekee ya kunifurahisha nijisikie raha kwamba nimefika kwa watani zangu ninao wapenda na wao kumbe wananipenda ni kunipa kura za kutosha,” amesema Dkt. Magufuli.