Magufuli Aweka Mpango wa Kujenga Bandari Nyingine Mwanza
0
September 07, 2020
Mgombea Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema ataangalia uwezekano wa kujenga bandari ya Mizigo wilayani Magu mkoani Mwanza iwapo atapewa dhamana ya kuongoza kwa miaka mitano mingine.
Magufuli alisema hayo wakati akizungumuza na wananchi wa Magu akiwa njiani kuelekea jijini Mwanza kunadi sera zake kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwezi oktoba mwaka huu.
Alisema endapo atapata nafasi ya miaka mitano mingine ataweka mipango kujenga bandari ya mizigo wilayani Magu kwani ni eneo lenye nafasi na lipo kando ya ziwa Victoria.
Alisema kukamilika kwa bandari ya Mizigo wilayani humo kutatoa fursa kwa meli zinazofanya safari ziwa Victoria kupitia bandari hiyo kushusha mizigo na kupunguza msongamano kwenye bandari ya zamani iliyopo jijini Mwanza.
Aidha Dk. Magufuli alisema atahakikisha anakamalisha usambazaji wa umeme kwenye vijiji vyote vilivyobaki havijapitiwa na umeme wilayani humo.
Alisema hadi sasa vijiji 9570 Tanzania nzima vimeshapitiwa na umeme huku vijiji vilivyosalia vikiwa ni 2600 ambapo miongoni mwake kuna vijiji 38 ambavyo havijaunganishiwa na umeme na kuahidi kuviunganishia vyote iwapo atapewa awamu nyingine tena.
Pia Dk. Magufuli aliahidi kuendeleza sera ya Tanzania ya viwanda kwa na kuahidi kujenga kiwanda cha kuchakata Pamba wilayani humo ili kusaidia kuongeza thamani ya zao la pamba ambapo badala ya kuuza marobota ya pamba sasa Tanzania itaanza kuuza nguo.
Alisema bado sera ya kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda inaendelea ambapo hadi sasa serikali imefufua jumla ya viwanda 8440 na kwenye awamu ijayo akichaguliwa tena ataongeza viwanda vingine ili kutoa fura ya ajira kwa watanzania.
Dk. Magufuli pia alisisitiza watanzania kuthamini na kuilinda amani ya taifa na kutodanganyika katika kipindi hiki cha uchuguzi na kuiingiza nchi kwenye machafuko kwani amani ndiyo msingi wa maendeleo.
Tags