'Magufuli Kaongeza Pato la Mwananchi Mmoja Mmoja, Kamaliza Changamoto ya Umeme' Mariam Ditopile
0
September 06, 2020
MITANO mingine kwa Magufuli! Ndicho ambacho Mbunge Mteule wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile alivyowaambia wananchi wa Jiji la Dodoma wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde.
Ditopile amesema miaka mitano ya kwanza ya Rais Dk John Magufuli imekua ya mafanikio kwa kila mtanzania kwa sababu amegusa kila sekta kuanzia uchumi, elimu, afya na miundombinu.
Amesema leo Tanzania inanufaika na rasilimali zetu wenyewe kwa sababu Magufuli ameamua kutanguliza maslahi ya watanzania hasa wanyonge ambao kwa kipindi kirefu wamekua wakiteseka kwa kuona Mali zao zinaibiwa.
" Kwa sasa tunanufaika na rasilimali zetu hasa madini, tuliona kwenye makinikia jinsi Jemedari wetu Magufuli alivyowatikisa wazungu hadi wakaja nchini na pesa wakatoa huku wakikubaliana na masharti ya JPM.
Wapinzani wakiongozwa na mgombea wao Urais wakapiga kelele kuwa tutashtakiwa haya waseme sasa tumeshtakiwa na nani? Wamebaki na aibu kwa sababu Magufuli amewaonesha nini maana ya kuwa Rais wa Nchi tena Tanzania," Amesema Ditopile.
Kuhusu uchumi Ditopile amesema Dk Magufuli ametekeleza kwa kiasi kikubwa ahadi yake ya kukuza uchumi ambapo ndani ya miaka mitano yake ya kwanza amekuza pato la mwananchi mmoja mmoja kutoka Sh Milioni 1,968,965 hadi Sh Milioni 2,45,496 ambao ni wastani wa asilimia 6.7 kiwango ambacho ni kikubwa kulinganisha na kipindi kingine chochote toka Uhuru.
Amesema siyo tu ukuaji wa pato la mwananchi mmoja mmoja pia uchumi wetu kama Nchi umekua kwa kiasi kikubwa ambapo sasa tumepanda hadi kufikia uchumi wa kati na kuwa miongoni mwa Nchi 10 Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa.
Ditopile amesema yote yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na miradi mikubwa iliyotekelezwa na Rais Magufuli ndani ya miaka mitano ya kwanza, kuanzia Reli ya Kisasa 'Standard Gauge', mradi mkubwa wa umeme wa Rufiji, Ujenzi wa Miundombinu ya Barabara hasa Fly over za Tazara na Ubungo ambazo zote hizo zimetoa Ajira maelfu kwa maelfu.
" Wananchi wa Dodoma anaesema Rais Magufuli hajafanya kazi inabidi tumkatae kwa sababu kazi kubwa aliyoifanya kwenye Nishati ya Umeme haijawahi kutokea, nyie ni mashahidi jinsi mlivyokua mnaichukia Tanesco kwa kukatakata umeme, leo hii tumeshasahau ukatikaji wa Umeme.
Siyo hivyo tu upatikanaji wa umeme umeongezeka kutoka Megawati 1,308 mwaka 2015 hadi megawati 1,602 mwwka 2020 huku usambazaji wa umeme vijijini ukiongezeka kutoka asilimia 16.4 mwaka 2015 hadi asilimia 67 mwaka 2020. Ni kusema kwamba Nchi hii kwa sasa Umeme kukatika ni suala la maajabu tushaondoka huko, " Amesema Ditopile.
Amesema sekta ya nishati imekua kutoka asilimia 4 hadi asilimia 14.2 ambapo wakati Magufuli anaingia madarakani ni vijiji 4,000 vilivyokua na umeme lakini wakati huu tayari vijiji 9,112 vinawaka umeme.
Amewataka pia wapinzani kumshukuru Magufuli kwa jinsi alivyomaliza changamoto ya ugonjwa wa Corona bila kufungia watu ndani kama walivyokua wakitaka wao jambo ambalo limewasaidia hata wao kwa kufanya mikutano wakati huu wa kampeni.
Tags