Mahakama ya Haki ya Afrika Mashaki inatarajiwa kuamua kesi inayopinga uhalali wa Yoweri Museveni kugombea tena urais wa Uganda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.
Mahakama ya juu zaidi ya Uganda iliidhinisha marekebisho ya katiba ili kuondoa ukomo wa miaka kwa wagombea wa urais.
Marekebisho ya katiba ya mwaka 2017 iliondoa kifungu cha sheria kinachowataka wagombea uraisi kuwa na umri wa chini ya miaka 75.
Hatua hiyo ilimruhusu rais Yoweri Museveni, ambaye ana umri wa miaka 75, kugombea mhula wa sita katika uchaguzi wa Januari mwaka 2021. Amekuwa madarakani tangu mwaka 1986.
Wakili Male Mabirizi aliwasilisha shauri katika mahakama ya Afrika Mashariki, iliyopo nchi jirani ya Tanzania, kupinga uamuzi wa Mahakama ya Juu Zaidi ya Uganda. Anataka kifungu cha ukomo wa miaka wa wagombea urais kilichotolewa katika katiba kirudishwe.
Katika nyaraka alizowasilisha mahakamani alisema marekebisho hayo ya katiba yalifanywa "katika mazingira ya vurugu baada ya jeshi la polisi kupelekwa kushika doria ndani na nje ya bunge ", kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Daily Monitor.