Makala: Urafiki, Aadui wa Osama Bin Laden na Marekani; Al-Qaeda na ‘Ushetani’


Na Josefly

“Alikuwa mtoto mwenye sura ya mvuto, mpole na mwenye nidhamu. Ilikuwa nadra kutazamana naye moja kwa moja machoni. Alikuwa na aibu, msikivu na neno lake halikutoka kinywani mwake bila mpangilio,” alisema Bi. Alia Ghanem, mama mzazi wa Osama Bin Laden, aliyekuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda akielezea maisha ya utotoni ya mwanaye, miaka nane baada ya kuuawa na makomando wa Marekani waliomsaka kila kona ya dunia kwa kipindi cha miaka kumi.

Kwa mujibu wa mama huyo ambaye amebarikiwa kuishi hadi leo, tangu alipomzaa mwanaye Osama, Machi 10, 1957 katika mji wa Riyadh nchini Saudi Arabia, aliiona baraka na neema kwenye maisha ya mwanaye. Kila alipokuwa akivuka rika moja, alionesha kuwa na upeo wa hali ya juu. Darasani alikuwa na akili za kipekee na alifanikiwa kumaliza Shahada ya Uchumi kwa ufaulu mzuri katika Chuo Kikuu Cha King Abdulaziz kilichoko Jiddah, Saudi Arabia.

Akiwa na umri wa miaka 20, alianza kuonesha makucha ya uwezo wake na alifanikiwa kuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa vijana chuoni kwake. Jina lake liliwafikia haraka wanasiasa na watu wenye harakati za itikadi kali ambao walimuona kama silaha ya kipekee wanayoweza kuitumia.

Osama hakuwahi kuijua njaa, alizaliwa kwenye familia ya kitajiri! Baba yake Mohammed bin Awad bin Laden, mzaliwa wa Yemen, alikuwa milionea mwenye ukwasi wa kusaza. Pia, alikuwa na uhusiano wa karibu na familia ya kifalme ya Saudi Arabia. Alianzisha na kumiliki kampuni ya kimataifa ya ujenzi ya Saudi Binladin Group. Hii ndiyo kampuni ambayo mwaka 2011 ilipewa zabuni ya kujenga jengo refu zaidi duniani linaloitwa ‘Jeddah Tower’ lililopo Jeddah, Saudi Arabia. Hadi sasa lina makampuni zaidi ya 537. Sasa usiulize Osama alipata wapi pesa, alizaliwa katikati ya fedha za kiarabu (Arab Money), na wanasiasa waliisikia harufu ya fedha wakasogea wakijua wakifanikiwa kumteka akili tu mambo yao yataenda vizuri.

Familia ya Bin Laden ilitengeneza ukwasi wa $5 bilioni kupitia sekta ya ujenzi; baadaye Osama alipewa urithi wa kati ya $25 milioni na $30 milioni. Osama naye alikuwa na makampuni ya ujenzi, akatengeneza pesa nyingi alizozitumia kwa fujo lakini bado hakukaukiwa. Kweli mtoto wa nyoka hawezi kuwa kenge!

Mama yake Osama anaamini kuwa mwanaye alikuwa malaika hadi pale alipokutana na wanasiasa pamoja na watu wenye itikadi kali za kidini waliompandikiza itikadi zao. Osama akabadilika kisirisiri kutoka kuwa ‘malaika’ hadi kuwa ‘shetani’ anayewinda na kuua maelfu ya wasio na hatia.

“Alikuwa kijana mzuri hadi pale alipokutana na hawa watu ambao walimvuruga akili (brainwash) kwa kutumia dini akiwa na umri wa miaka 20. Niligundua, nikamuonya, alinipenda sana na hakutaka kuona naumia kwahiyo hakuwahi kukiri mbele yangu alichokuwa anafanya,” Mama Osama aliiambia The Guardian katika mahojiano maalum mwaka 2018.



Alimtaja Abdullah Azzam, kiongozi wa kundi la itikadi kali la Udugu wa Kiislam (Muslim Brotherhood) kuwa ndiye aliyemvuruga ubongo Osama kwakuwa aligeuka kuwa mshauri wake mkuu.

Baada ya kumaliza chuo kikuu mwaka 1979, somo la itikadi kali lilimkolea kichwani kuliko masomo ya chuo kikuu. Aliyachanganya yote na kuamua kwenda nchini Pakistan alikojiunga na wapiganaji wa Mujahideen kupigana na vikosi vya Umoja wa Kisoviet katika vita ya kuikomboa ardhi ya Afghanistan dhidi ya uvamizi wa vikosi vya Urusi.

Osama alitumia pesa zake kununua silaha nzito na kusaidia mafunzo ya kijeshi ya askari waliojitolea kutoka nchi mbalimbali za kiarabu kujiunga na Mujahideen. Na hapa ndipo kilipo kitendawili ambacho Marekani inakiruka futi 100, kuhusu kumsaidia Osama bin Laden au kuwahi kufanya kazi na jamaa huyu ambaye aligeuka kuwa mwiba wenye sumu kali dhidi ya Marekani na kila rafiki wa Marekani.

Tuhuma za Marekani kumsaidia Osama
Ni hivi… wakati Osama anawasaidia Mujahideen kupigana na vikosi vya Umoja wa Kisoviet na Serikali waliyoisimika ya Afghanistan, Marekani nayo kama kawaida yake kusaidia adui wa adui yao kwa jina la oparesheni demokrasia au oparesheni rejesha haki ili kumpiga adui yao, wakati huo waliita ‘Operation Cyclone’… wakamwaga misaada ya kila aina kwa Mujahideen ili kuhakikisha majeshi ya Kisoviet yanachakazwa vibaya Afghanistan. Kumbe walimfuga mamba amtafune adui yao bila kujua atapata njaa wakati ambapo adui huyo hayupo na itakuwa zamu yao!

Tena, inadaiwa kuwa Shirika la Kijesusi la Marekani (CIA) lilimsaidia Osama Bin Laden kujenga handaki lililotumika kama ngome ya maficho ya mafunzo ya wapiganaji wa Mujahideen yanayofahamika kama ‘Khost’ yaliyokuwa Afghanistani. Ni maficho hayahaya ambayo Marekani iliyashambulia vikali baada ya shambulizi la kigaidi la balozi za Marekani nchini Tanzania na Nairobi, hatua ambayo inadaiwa kuamsha hasira zaidi za Osama na kupanga shambulizi la Septemba 11.

Mwaka 2004, BBC kwenye Makala yao ya ‘Al-Qaeda’s origins and links’ waliandika “wakati wa vita dhidi ya Soviet, Osama bin Laden na wapiganaji wake walipokea misaada kutoka Marekani.” Wachambuzi wengine wanaamini CIA walimpa Osama mafunzo ya ulinzi. Mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia, Bandar bin sultan aliwahi kusema kuwa Osama alimshukuru kwa juhudi zake za kuwaleta Marekani kusaidia Mujahideen kukomboa ardhi ya Afghanistan.

Robin Cook, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza kati ya mwaka 1997 na 2001, aliandika “Osama alikuwa zao la makosa makubwa ya mahesabu ya idara za usalama za Magharibi. Katika miaka ya 1980 alipewa silaha na mafunzo na CIA pamoja na Saudi kupigana vita dhidi ya vikosi vya Urusi vilivyokuwa Afghanistan.”

Hata hivyo, madai hayo yalipingwa vikali na Marekani. Wao wanasema walikuwa wanawasaidia Mujahideen ambao ni wazawa wa Afghanistan na sio wale wapiganaji wageni kama Osama Bin Laden; na kwamba hakuna hata afisa mmoja wa CIA ambaye aliwahi kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na Osama Bin Laden au Al-Qaeda.

Osama alianzisha kundi la kigaidi la Al-Qaeda mwaka 1988 akiwa Afghanistan. Alishirikiana na rafiki zake akiwemo raia wa Misri, Ayman Alzawahiri na Abdullah Azzam. Hapo ndipo yule malaika alipogeuka na kufanya matendo ya kishetani, akiwinda damu za wasio na hatia kwa mwamvuli wa vita ya imani (Jihad).



Alirejea nyumbani kwao Saudi Arabia akitoka Afghanistan na kupokelewa kama shujaa wa vita ya Jihad, baada ya Mujahideen kufanikiwa kuwafurusha Wasoviet (Warusi). Hata hivyo, uwepo wake nchini Saudi Arabia, uligeuka kuwa mwiba dhidi ya himaya ya Kifalme ambayo ilikuwa rafiki wa karibu wa baba yake.

Osama aliushawishi utawala wa Kifalme kukataa misaada ya kijeshi ya Marekani na akawataka waviondoe vikosi vya Marekani nchini humo ili ardhi hiyo Takatifu yenye majiji ya Mecca na Medina ilindwe na vikosi vya kiislam. Aliahidi kutoa msaada wa kijeshi kuisadia Saudi Arabia kuvifurusha vikosi vya Iraq vilivyoivamia Kuwait na kuwa tishio kwa nchi hiyo badala ya kuwatumia Marekani.

Hata hivyo, ushawishi wake uligonga mwamba. Baada ya himaya ya kifalme kumgomea, akaanza kuupinga utawala wa kifalme hadharani.

Kufuatia hatua hiyo, Utawala wa kifalme ukamuandama na mwaka 1990 alikimbilia Sudan. Saudi Arabia ilimvua uraia mwaka 1992. Kuanzia mwaka huo akawa hana uraia wa nchi yoyote. Alikaa Sudan kwa kipindi cha miaka minne, akajenga himaya na kufanya kazi kubwa za ujenzi wa miundombinu za Serikali na kutoa misaada mingi kwa wananchi. Marekani ilishinikiza Serikali ya Al-Bashir kumkamata Osama na kuwakabidhi.

Alipona majaribio kadhaa ya kutaka kuuawa na watu ambao alidai wametumwa na Marekani pamoja na Saudi Arabia.

Baada ya kugundua Al-Bashir ameanza kukubaliana na presha ya Marekani akiogopa kutumbuliwa, Osama aliondoka nchini humo kwa msaada wa ulinzi wa makomando wa Afghanistan iliyokuwa inatawaliwa na rafiki yake, Mullah Omar, mpiganaji wa Mujahideen ambaye alikuwa anaongoza serikali ya nchi hiyo akiwa ameanzisha vuguvugu la wapiganaji wa Taliban (Islamic Emirate of Afghanistan).

Alipofika Afghanistan akiwa chini ya mwanvuli wa Mullah Omar, akatangaza vita dhidi ya Marekani. Akaanzisha mashambulizi mengi ya kigaidi dhidi ya Marekani na rafiki zake. Mwaka 1998 baada ya mashambulizi ya balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya, Marekani ilimuweka Osama kwenye orodha ya watu 10 wanaotafutwa na FBI, na wakamtaja kuwa ndiye gaidi anayetafutwa zaidi duniani.

Marekani haikukubali fedheha, uchokozi na udhalimu wa Al-Qaeda. Ilijibu haraka kwa kumuadhibu vikali Osama na Al-Qaeda yake. Ilishambulia maficho ya mahandaki ya ‘Khost’ huko Afghanistan kulikokuwa na kambi za mafunzo za Al-Qaeda na Taliban. Maficho ambayo yanadaiwa kuwa yalijengwa kwa msaada wa Marekani enzi zile za Mujahideen inawapiga Wasoviet.

Kilikuwa kipigo kikali kuwahi kutokea dhidi ya Al-Qaeda. Walikimbia hovyo, damu isiyo na hatia waliyoimwaga Dar es Salaam na Nairobi iliwagharimu.

Siku chache baadaye, mwandishi wa CNN, Peter Arnett aliyewahi kupata nafasi ya kufanya mahojiano na Osama Bin Laden, anasema alipokea simu aliyopigiwa na Al-Zawahir, ambaye alimwambia kuwa yuko karibu na Osama na kwamba anaomba amfikishie ujumbe Rais wa Marekani wakati huo, George Bush kuwa atalipa kisasi kwa mtindo utakaoandika historia.

Septemba 11, 2001, Jumanne tulivu, iligeuka kuwa siku iliyotengeneza maumivu makali kwa Marekani. Ndege za nchi hiyo zenye raia wake na raia wa kigeni ziliingia mikononi mwa wapiganaji wa Al-Qaeda waliojifanya kuwa ni abiria wema. Watu hao waliojitoa mhanga waligongesha ndege hizo kwenye majengo ya Makao Makuu ya Idara ya Ulinzi (Pentagon) pamoja na Jengo la Kituo cha Biashara cha Dunia (World Trade Center complex) lililopo Manhattan. Zaidi ya watu 2,996 wasio na hatia walipoteza maisha na wengine 6000 walijeruhiwa.


Shambulizi la Septemba 11, 2001 kwenye majiji ya New York na Washington

Hili lilikuwa tukio moja la kigaidi lililosababisha vifo vingi zaidi kwenye historia. Tukio hilo lilisababisha hasara ya $10 bilioni ya ukarabati wa miundombinu tu.

Ingawa awali Al-Qaeda walikana kuhusika na tukio hilo, Marekani ilimtaka Mullah Omar kuwakabidhi haraka Osama Bin Laden na alipokaidi walimuadhibu vikali. Walishusha makombora mazito Afghanistan dhidi ya Taliban na Al-Qaeda. Kipigo hicho kiliwaondoa Taliban kwenye Serikali na kuwafanya kuwa kundi la wapiganaji tu, yaani kama waasi. Mwaka 2004, Osama alikiri kwenye kipande cha video kuwa ndiye aliyepanga shambulizi la Septemba 11 na akadai lengo ni kuhakikisha anawafilisi Marekani na marafiki zake na kuwamaliza.

Marekani ilitangaza zawadi nono kwa atakayefanikisha kupatikana kwa Osama Bin Laden. Rais George Bush alieleza kushtushwa na tukio hilo na akaahidi kutumia gharama zozote kumkamata mhusika.

“Marekani imevijua vita, lakini kwa miaka 136 imekuwa ikipigana nje ya ardhi yake. Marekani inajua majeraha ya vita lakini sio katikati ya majiji yake makubwa. Tunayajua mashambulizi ya kushtukiza lakini sio mbele ya maelfu ya wananchi wetu… haya yote yameletwa kwetu siku moja tu tena asubuhi tulivu,” alisema Rais Bush akiwahutubia wananchi kufuatia tukio hilo, akiahidi kutolala hadi wamkamate Osama Bin Laden na wenzake.

Ingawa kwa waswahili za Mwizi ni Arobaini, kwa Wamarekani za mwizi hazihesabiki, na zikifika ni zaidi ya filamu ya Arnold Schwarzenegger, Commando John.

Lile fupa lililomshinda Bush akalitupia kwa Barack Obama, kiongozi wa kwanza mweusi kuongoza taifa hilo mwenye asili ya Kenya. Mjaluo yule akachanganya na ujanja wa kizaramo wa kumfukuza mwizi kimyakimya.

Mei 2, 2011, Rais wa Marekani, Barack Obama alionekana mchana Ikulu akiwa amejaa tabasamu na bashasha. Jioni, alionekana akiwa anacheza golf, kwake ilionekana kuwa ni siku laini kuwahi kutokea na kama vile alikuwa mapumzikoni.

Kumbe dakika zilikuwa zinahesabika, viongozi wa Marekani waliopita walialikwa Ikulu kuangalia filamu mpya. Hawakujua ni filamu gani, lakini walisisitizwa kufika bila kukosa. Ilipofika majira ya saa saba usiku, screen ziliwashwa. Ndipo Rais Obama alipowajuza waalikwa wake kuwa wataona ‘mubashara’ tukio la kumkamata au kumuua Osama Bin Laden. Unaambiwa kabla ya hapo, ni kundi la watu wasiozidi wanne ndilo lililokuwa linajua, hata mke wa Obama mwenyewe hakujua nini kinaendelea.


Viongozi wa Marekani wakiangalia mubashara tukio la kumuua Osama Bin Laden, Ikulu

Kwa upande mwingine, wachezaji wa filamu hiyo, Kikosi maalum cha Marekani, chenye makomando kilifanya mazoezi kwa siku kadhaa nchini Afghanistan bila kujua kinaenda kumuua nani hasa. Kilipewa jina la Osama Bin Laden sekunde 30 tu kabla ya kuingia kwenye ndege na kuanza safari kuelekea kazini.

McRaven, aliyekuwa Kiongozi wa vikosi maalum vya ‘Navy SEAL’ndiye aliyekuwa na siri nzito kutoka Ikulu. Ndiye aliyemshauri Obama kuchukua uamuzi mgumu wa kupeleka makomando bila kuiambia Serikali ya Pakistan, huku nyuma aliandaa vikosi vya kuwaokoa makomando hao kama wakikutana na kizingiti cha jeshi la Pakistan.

Majira ya saa saba usiku, makomando hao walivamia makazi ya maficho ya Osama Bin Laden yaliyokuwa Abbottabad nchini Pakistani na kufanikiwa kumuua. Kweli, kutojua kulimfanya jogoo mwenye njaa kulala na mende usiku mzima bila kubaini alilala na chakula… Osama alikutwa katika jengo moja karibu na makazi ya jeshi la Pakistan, hali iliyosababisha malumbano kuwa huenda alikuwa anatunzwa na Serikali ya Pakistan.


Makazi ya Osama Bin Laden, Abbottabad, Pakistan

Kutokana na teknlojia ya aina yake, rada za Pakistan hazikuweza kunasa ndege za kijeshi za Marekani zilizoingia nchini mwao na hawakufahamu lolote hadi kazi ilipokamilika.

Huko Ikulu ya Marekani ‘White House’, watazamaji wa filamu hiyo walikuwa wanashangilia kama watu walioongezewa kifurushi cha ‘halichachi’ au ‘maisha bila kikomo’.

Risasi iliyofyatuliwa na komando Rob O’Neill ndiyo iliyomuua Osama Bin Laden. Cha kushangaza, miaka michache baadaye komando huyu aliacha kazi ya jeshi na kuamua kuwa mzungumzaji mhamasishaji (motivational speaker). Sababu hazijulikani, na aliwahi kuonywa kuzungumzia siri zozote za oparesheni alizoshiriki. Aliachana na jeshi kwa hiari miaka 16 baada ya kulitumikia badala ya miaka 20 aliyokuwa anatarajiwa kustaafu.



Huo ukawa mwisho wa Osama Bin Laden. Hakuna aliyeuona mwili wake. Inadaiwa kuwa alizikwa kwa heshima baharini kwa kuzingatia imani ya Kiislam. Lakini nani wa kuamini hilo? Hata kuamini kama aliuawa kweli ni hadi mwanaye Hamza Bin Laden na kundi la Al-Qaeda walipothibitisha.

“Mabibi na mabwana, leo usiku, vikosi vya Marekani vimefanya oparesheni iliyofanikiwa kumuua Osama Bin Laden, kiongozi wa Al-Qaeda,” Rais Barack Obama alizungumza kwa furaha kupitia hotuba yake ya dharura kwa taifa hilo.

Ingawa Osama alikuwa na majeshi yaliyoisumbua Marekani na kuisaidia Mujahideen kupiga vikosi vya Urusi nchini Afghanistan, alikutwa akiwa kwenye nyumba yenye ghorofa mbili ndogo yenye vitanda tisa tu vya kulala na walinzi takribani sita tu.

Nyumba yake ilikuwa na wakaazi 17 na haikuwa na simu au runinga au hata CCTV camera. Ilikuwa na compyuta moja tu aliyoitumia kuandika jumbe mbalimbali kwa watu wake. Hakukuwa na Internet, jumbe hizo zilipelekwa mkono kwa mkono na wafuasi wake watiifu zaidi. Aliishi na familia yake na wake zake wawili na baadhi ya watoto wake waliozaliwa katika jengo hilo walikuwa naye usiku huo alipouawa.

Kutokana na umaarufu wa kihalifu wa umwagaji damu, Serikali ya Pakistan ilivunja nyumba ya Osama ili isigeuke kuwa sehemu ya makumbusho.

Ameacha zaidi ya watoto 20 na alikuwa na wanawake wanne. Watoto wake wengine wanaishi nchini Marekani.



Richard Clarke, Afisa wa zamani wa Ulinzi wa Taifa wa Marekani alisimulia kuwa vikosi vya Marekani vilikuta kompyuta aliyokuwa anaitumia Osama na kwamba ilikuwa na mpango wa shambulizi lingine la kumbukizi ya miaka 10 ya Septemba 11. Alisema shambulio hilo lilikuwa linalenga treni za umeme za Marekani. Kutokana na taarifa hiyo, walifanikiwa kulizima.

Kijiti cha uongozi wa Al-Qaeda kikapokelewa na rafiki yake mkuu, Ayman al-Zawahiri. Marekani ikatangaza donge nono la US$25 milioni kwa atakayesaidia kupatikana kwake.

Lakini pia, mtoto wa Osama, Hamza Bin Laden ambaye sasa ana umri wa miaka 29 ndiye anayeonekana kuja kuridhi mikoba ya baba yake. Marekani imetangaza dau la $1 bilioni kwa atakayesaidia kumpata Hamza ambaye ni nyoka kama baba yake.

Nani wa kuponda kichwa cha Al-Qaeda na makundi ya kigaidi ili dunia iwe sehemu salama zaidi? Majeshi hayataweza bila ushirikiano wa kila mwenye nia njema kuiondoa imani potofu kwenye vichwa vya kizazi hiki inayowageuza waliozaliwa malaika kuwa mashetani.

Hakuna aliye salama kwani kwa imani potofu ya magaidi, kumuua mtu asiye na hatia aliyesimama karibu na adui yako sio kosa!!!

Kwa mujibu wa CIA na FBI, Magaidi wamewekeza ngome zao katika nchi zaidi ya 60 duniani kote, wakipanga kuua watu wasio na hatia. Al-shabaab, Boko Haram, ISIS na makundi mengine yanayotumia mwamvuli wa itikadi kali kuondoa maisha ya wasio na hatia yanapaswa kupigwa vita na kila mwenye pumzi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad