AJALI haina kinga! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia tukio la msanii wa muziki wa kizazi kipya, Abdul Rajab ‘Harmonize’ kuanguka wakati akitua kwa kutumia kamba maalum (zipline) ndani ya Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam wikiendi iliyopita.
JINSI ILIVYOKUWA
Mashabiki na wadau wa Klabu ya Soka ya Yanga, walikuwa kwenye kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Mwananchi yaliyofanyika uwanjani hapo huku burudani mbalimbali ziliupamba uwanja huo uliokuwa umefurika umati wa watu.
Mbali na mtanange wa soka kati ya Yanga na Aigle Noir ya Burundi kusubiriwa na mashabiki, uliwadia wasaa wa Harmonize kuingia uwanjani hapo kwa ajili ya kutumbuiza ambapo kwa ufundi mkubwa aliingia kwa kutumia Zipline jambo lililowafanya maelfu ya mashabiki wa Yanga kushangilia.
Harmo kwa kujiamini na madaha kibao alishuka uwanjani hapo kijeshi, akitokea juu ya paa la uwanja huo huku akiwa kwenye mavazi ya mabakamabaka kama mwanajeshi. Wakati Harmo akiendelea kushuka na kamba hiyo maalum alipobakiza mita kadhaa kabla ya kutua chini, tukio lisilo la kawaida lilitokea.
Ghafla alionesha ni kama amepoteza mwelekeo, akaporomoka kwa kasi kubwa kutoka umbali wa futi kadhaa na kujipigiza chini kabla ya kamba aliyokuwa akiitumia ikamrudisha tena juu!
Sintofahamu ya anguko lake ilipokuwa likiendelea wasaidizi wake waliokuwa jirani na eneo hilo walienda kumuokoa kwa kumnasua kutoka kwenye kamba ambayo ilikuwa bado inamshikilia mwilini.
“Atakuwa kaumia jamani,” na maneno kama hayo yalianza kujitokeza miongoni mwa mashabiki waliokuwa wakisubiri uhondo wa shoo yake lakini mwisho wa siku Harmo alianza kuangusha shoo na kuifanya mioyo ya watu ikome kupwita.
MAKOSA YA KIUFUNDI
Uchunguzi wa RISASI MCHANGANYIKO uliohusisha vyanzo mbalimbali mitandaoni na mmoja wa wataalam wa Zipline nchini unaonesha kuwa huwenda kuna makosa ya kiufundi yalitokea wakati msanii huyo akishuka.
“Ukiangalia video utaona jinsi Harmo alivyoporomoka ghafla na kuanguka, kwenye huo mchezo kuna kanuni zake ambazo zinamhusu mtumiaji na nyingine zinawahusu wanaomuongoza.
“Kukitokea kosa kati ya pande mbili mtu huanguka, kama Harmonize angekuwa kenye umbali mrefu huwenda angekufa na wengi wamekufa katika mchezo huu, nenda kaangalie kwenye mitandao abonyeze taratibu kifaa hicho, ukiwatazama makomando au wanajeshi, wanapokuwa wanatua, hupendelea zaidi staili ya kutumia ‘breki’ moja pekee ya kupunguza kasi unayokuwa nayo mtu unapokuwa hewani.
“Wakikaribia kugusa ardhi, huwa wanajiandaa kukimbia kidogo ili kuendana na kasi waliyotoka nayo juu, haya ni mambo ya kitaalamu zaidi.
“Sasa kwa Harmonize, kama angetumia breki ya kawaida pekee bila kugusa ile breki ya dharura, pengine yasingetokea kama yaliyotokea, angeendelea kushuka na akikaribia kugusa uwanja.
“Angejiandaa na kukimbia kidogo kwa miguu ili kumaliza kasi aliyotoka nayo juu, lakini hilo halikufanyika,” alisema.
Aliongeza kuwa matatizo mengine yanayoweza kusababisha ajali katika mazingira kama yale ni pamoja na mhusika kuwa na hofu kubwa, kitaalamu inaitwa ‘fear of heights’ pamoja na matatizo katika mfumo mzima wa uendeshaji zipline. Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, chanzo kingine cha ajali za aina hiyo, huwa ni hitilafu kwenye mfumo wa waya zinazotumika kwenye ‘usafiri’ huo.
“Nimeelezea hisia zangu kwa Harmonize pengine ndiyo alifanya makosa lakini anaweza asiwe yeye na tatizo likawa lilianzia kwenye mfumo mzima na hivyo yeye akajikuta hawezi kujitetea.
“Kwa kawaida nyaya hizo huwa hazifungwi kienyeji, zinafungwa na wataalam na kwa hapa nchini wengi wapo jeshini,” alisema.
“Ukitazama kwa pale uwanjani, nyaya zilikuwa zimefungwa vizuri ndiyo maana kuanzia mwanzo Harmonize alionekana akishuka taratibu bila tatizo lolote, hiyo inaonesha kwamba kazi ilikuwa imefanywa na wataalam waliobobea.
“Dosari nyingine ambayo huweza kusababisha ajali kwa watumiaji wa zipline, ni kufyatuka kwa ‘spring’ za breki! “Inapotokea kwa sababu yoyote ile zikafyatuka, maana yake ni kwamba kasi ya kushuka chini itaongezeka ya kijamii utanaona klipu za video,” alisema mtaalam mmoja ambaye amepata kupitia mafunzo ya kijeshi lakini hakupenda kutajwa jina lake gazetini.
Aliongeza kuwa makosa yaliyotokea kwa Harmo, huwatokea watumiaji wengine wa Zipline, chanzo kikiwa ni kukosa uzoefu na elimu sahihi juu ya namna ya kutumia kifaa hicho. “Kwenye kile kifaa anachovaa mtu kiunoni hadi kifuani sambamba na mabegani kwa baadhi ya watu, kunakuwa na kamba au mikanda migumu ambayo kazi yake inakuwa ni kuhakikisha usalama wa mtu awapo angani.
“Mikanda hii hutumika ku-balance uzito wa mwili sambamba na kubalansi kasi anayoitumia mtu awapo angani. “Kwenye mikanda hiyo, kunakuwa na ‘lock’ mbili ambazo zimetengenezwa kwa chuma kigumu, hizi ndizo zinazotumika kumfanya mtu aning’inie kwa usalama, abembee kwenda mbele kwa kasi, asimame kawaida au pale kunapotokea dharura,” alisema mtaaam huyo.
Aidha, anaendelea kueleza kwamba kwenye hizo lock mbili, ile inayomuwezesha mtu kutereza juu ya kamba huwa na kifaa ndani yake ambacho hutumika kama breki.
“Lakini pia mbali na breki ya kawaida, kuna kifaa kingine ambacho kitaalamu huitwa emergency arrest device (EAD), hiki hutumika pale mtu anapotaka kusimama au kutua kwa dharura pekee.
“Ukitazama vizuri tukio la Harmonize, utaona kwamba alikuwa anaelekea kutua vizuri tu lakini ghafla ni kama aligusa kifaa ambacho kwa uelewa wangu nahisi ni EAD.
“Ingawa haioneshi vizuri lakini hisia zinaakisi kwamba baada ya kugusa kifaa hicho tu ndipo alipoporomoka kwa kasi mpaka chini.
“Kiufundi hakutakiwa kuruhusu kushuka kwa nguvu alitakiwa maradufu na kama mhusika hana uwezo wa kutumia breki za dharura (EAD), uwezekano mkubwa ni kwamba anaweza kupata madhara makubwa ikiwemo kifo.
MADHARA
Ajali za zipliner, kama zilivyo ajali nyingne za vyombo vya usafiri, huwa na madhara makubwa ikiwemo kifo. “Kilichomsaidia Harmonize ni kwamba mgongoni alikuwa na begi ambalo pale alipoanguka, lilitoa ‘support’ kwake, angeweza kujibamiza kichwa na kupata madhara makubwa zaidi ikiwemo mtikisiko wa ubongo, kuvunjika mbavu na kadhalika! Ni jambo la kumshukuru Mungu kwamba yupo salama,” alisema mtaalam huyo.
MWENYEWE ANASEMAJE?
RISASI lilimtafuta Harmonize bila mafanikio kwani simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa, baadaye akatafutwa meneja wake, Beauty Mmari ‘Mjerumani’ ambapo alipopatikana, mazungumzo yake na mwandishi wetu yalikuwa kama ifuatavyo:
Risasi: Hongera kwa shoo nzuri iliyofanywa na msanii wako. Meneja: Ahsante sana, tunashukuru mashabiki kwa jinsi walivyotupokea.
Risasi: Kulitokea hali ya sintofahamu wakati Harmonize akiwa anatua. Vipi kuna madhara yoyote ya kiafya aliyoyapata?
Meneja: Hakupata madhara yoyote na ndiyo maana utaona kwamba baada ya tukio lile, aliendelea kupafomu vizuri. Kama angekuwa amepata madhara yoyote asingeweza kuwafurahisha mashabiki kama alivyofanya, tena kwa muda mrefu vile.
Pia baada ya kumaliza kupafomu alikuwa na ‘after party’ ofisini kwake na tulikuwa ‘live’ kwenye akaunti za mitandao ya kijamii.
“Hivi tunavyozungumza, Harmonize yuko salama kabisa na anaendelea na majukumu yake ya kama kawaida,” alisema meneja huyo.