Mashindano ya mbio za magari kuanza septemba 19 Iringa




 MASHINDANO ya mbio za magari ya ya Iringa Rally 2020  yanatarajia kutimua vumbi mjini Iringa Septemba 19  na kushirikisha timu zipatazo 19 kutoka mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi.

Akizungumza na Wanahabari mkoani Iringa Msimamizi wa Mashindano ya Iringa Rally, Hidaya Kamanga alisema maandalizi ya mashindano hayo yamekwisha kamilika kwa asilimia 95 ambapo hadi kufika siku ya tukio maandalizi yote yatakuwa yamekwisha kamilika.


Alisema kuwa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano hayo imejipanga kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa ukamilifu na kuleta Burudani kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa ambapo yamekuwa yakileta msisimko kwa mashabiki wa mbio za magari.


Alisema kuwa washiriki mbalimbali 19 wamekwishakamilisha taratibu zote za kushiriki mashindano hayo ambayo yamedhaminiwa na makampuni mbalimbali na wadau wa mbio za magari ambapo madereva wengi waliothibitisha hadi sasa wanatoka Tanzania, akiwemo bingwa wa mashindano hayo mwaka jana Ahmed Huwel ambaye amepania kwa kiasi kikubwa kuibuka bingwa wa mashindano hayo msimu huu.


Aliwataja madereva wanaotarajia kushiriki mashindano hayo kuwa ni Randeep Sigh amnbaye atashirikiana na Zubairy Paredina kutoka timu ya Bird Rally, Gurpa Sandhu na Dave Sihoka kutoka timu ya AESL Racing, Manveer Bird na Ravi Chana kutoka Birdi rally Team,  kutoka Siera Zullu team ni Altaf Munge na Ally Hamoud.


Wengine watakaoshiriki mashindano hayo ni kutoka timu ya Munge rally Team,Tylor Rally Team, Juakali Rally Team, TRT/Juakali rally Team,Hari Singh Team A, Hari  rally Team B, Hari Rally Team C, Mkwawa Rally Team na Siera Zullu Team.


Team nyingine ambazo zitashiriki mashindano hayo, ni Vulaa rally Team, Siera Rally Team B, mshiriki Fayaz Imran Chandu na Mkwawa rally Team chini ya bingwa wa mashindano hayo Ahmed Huwel akishirikiana na Rahim Suleiman.


Mashindano hayo yanatarajia kuwa ya aina yake kutokana na maandalizi yake kuwa mazuri na wananchi kuyasubiri kwa hamu katika njia yatakayopita ambazo safari hii yataanzia kwenye kituo cha mafuta cha Hope kisha kwenye hotel ya kitalii ya Mount Royal ambapo yatahusisha km 105.


Kwa upande wake mwenyekiti wa mashindano hayo, Amjad Khan aliwataka  wananchi  kujitokeza kwa  wingi  kushuhudia  mashindano hayo ila  kuwa makini na zaidi kwani mashindano ni mashindano na  magari  yanaweza kukosea  njia  hivyo si vizuri  kukaa jirani na barabara  badala  yake  kuchukua tahadhari wakati wa  kushuhudia mbio  hizo  za magari .


Aidha Khan alisema kuwa unapokuwa kwenye eneo la njia zinapofanyika mbio za magari kuwa makini, mwangalifu kwani waandaaji hawatakuwa na dhamana yoyote pindi ikitokea ajali kwa wananchi hao.


Aliongeza kuwa mtu yoyote hatakiwi kwenda na mtoto katika mashindano hayo na mama mjamzito hawaruhusiwi kuangalia mashindano hayo na wananchi kuwa makini katika maeneo ya kona ambapo gari zinapita


Naye Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Iringa, Yusuph Kamota aliwataka wananchi kuwa makini na mashindano hayo kwani ni hatari endapo itatokea ajali wakati wa mashindano na kuongeza kuwa mashindano hayo ni burudani kama zilivyo nyingine ila ni muhimu kwa wananchi kuwa makini.


Kamota alisema kuwa jeshi la polisi mkoani hapa limejipanga vyema katika kuimarisha ulinzi na Usalama katika Mashindano hayo ili yaweze kumalizika salama na kuwatakia mashindano mema washiriki wa mashindano hayo makubwa kabisa nchini.


Mashindano hayo yanadhaminiwa na wadau mbalimbali ikiwemo Hotel ya Mount Royal Iringa na mdhamini wa mashindano hayo miaka ya nyuma Maji ya Mkwawa, Camel Unga wa Ngano, Mgahawa wa The Koffee Shop, Kampuni ya Famari, Sunset Hotel, Sai Villa Hotel, Tosti, Alawi Mdee, Azam Tv, na Planet 2000 computer

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad