Baada ya Mchezaji wa Tanzania Mbwana Samatta kusajiliwa na Club ya soka ya Uturuki ya Fenerbahce, millardayo.com imepita kukusanya maoni ya Wadau mbalimbali wanaolifatilia soka kujua wamepokeaje hatua hiyo ya Mbwana kuondoka kwenye Timu inayocheza Premier League Uingereza ambapo tunae Mtangazaji Hodari Salim Kikeke.
“Fenerbahce ni Taasisi sio ya soka pekee ukitizama ina Timu za Riadha, Basketball, kuogelea, volleyball ni Taasisi kubwa sana, wanashikilia rekodi ya kushinda Ubingwa wa Uturuki kwa karibu mara 28 niimani yangu kwa Uturuki Samatta atacheza kama alivyokuwa anachezeshwa Genk” – Kikeke
“Kwa mtazamo wangu Samatta amepanda ngazi japo ametoka kwenye Ligi ambayo ni maarufu sana Duniani lakini anakwenda Uturuki katika timu ambayo inacheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, tusishangae kuona msimu ujao Fenerbahce wanakuja hapa England kucheza Ligi ya Mabingwa na Tottenham, Liverpool au Arsenal au Man City kitu ambacho kilikuwa ni ndoto ya mbali sana kwa Aston Villa kuweza kumaliza hata katika nafasi ya 10 (EPL)”
“Mfumo wa Kocha Dean Smith Aston Villa ulikuwa tofauti kwa sababu hakutaka kumchezesha Mbwana Samatta kama Striker pekeyake alikuwa anamchezesha zaidi asaidiane na Wachezaji wengine pale mbele tofauti kabisa na jinsi alivyozoea, inawezekana kabisa mfumo haukuwa umemfaa Samatta ukilinganisha na jinsi alivyokuwa yeye mwenyewe akiamua anacheza vipi wakati yuko Genk”
“Kusema kweli kwa mtazamo wangu hakupata muda wa kutosha amehamia Uingereza mwezi wa kwanza, halafu miezi miwili baadae kukaingia janga la Corona, Ligi ikasimama na yeye yupo kwenye Nchi ngeni ndio amehamia tu hajafahamu mazingira yake na hajafahamu Watu” asema Kikeke
“Kingine kama ukitazama hakupata muda wa kucheza wa kutosha sikumbuki mechi yoyote ambayo amecheza dakika 90 alikuwa akiingia anawahi kutoka au anaingia kama Sub ukitizama Genk alikotoka alikuwa akipiga dakika 90 zote”