Mazungumzo ya amani kati ya wajumbe wa Taliban na serikali ya Afghanistan yameendelea tena leo, ambapo jitihada za utafutaji wa kusitisha mapigano ya kudumu ni moja ya masuala kadhaa muhimu katika majadiliano hayo.
Katika hafla ya ufunguzi hapo jana mjini Doha, Qatar kulishuhudiwa serikali ya Afghanistan, na washirika wao ikiwemo Marekani, wakitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano.
Lakini Talibaan, ambayo imekuwa ikishiriki vita vya msituni, tangu iondolewe madarakani kwa nguvu 2001, haikuzungumzia kusitisha mapigano wakati wakirejea katika meza ya mazungumzo.
Lakini mkuu wa mchakato wa amani wa serikali ya Afghanistan, aliliambia shirika la habari la AFP, kwamba Taliban wanaweza kutoa fursa ya kusitishwa mapigano kwa makubaliano ya kuachiwa zaidi kwa wapiganaji wake walioko magerezani.