KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck amefunguka kwamba straika wake, Meddie Kagere anakaa benchi kutokana na yeye kupanga na kuchagua timu kutokana na aina ya timu ambayo anaenda kukutana nayo kwenye mechi zao.
Kocha huyo ameongeza kwamba pia amekuwa akiangalia zaidi mafanikio ya timu yake katika kushinda na wala siyo mtu mmoja huku kila mchezaji aliye hapo anaweza kukaa benchi kutokana na atakavyokuwa anawaona wapinzani wake.
Kagere ambaye alikuwa mfungaji bora wa timu hiyo kwa msimu uliopita, amekuwa akikosa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo ikiwemo katika mechi ya Ngao ya Jamii mbele ya Namungo FC ambapo Simba walishinda mabao 2-0.
Sven amesema kwamba hakuna tatizo la Kagere kukaa benchi ndani ya timu hiyo kutokana na hali hiyo inaweza kumkuta mchezaji yeyote ndani ya kikosi hicho kwa sababu ya kuangalia mafanikio zaidi ya kikosi hicho kuliko mtu binafsi.“Kuhusiana na Kagere wala hakuna tatizo lolote lile la yeye kukaa benchi kwa sababu hilo linaweza kumtokea kila mchezaji aliye hapa.
“Nachagua timu kutokana na mfumo ulivyo na namna tunavyocheza, sijui kwa nini watu wanazungumzia kuhusiana na mtu mmoja.
“Naangalia mafanikio zaidi ya timu, kama tunashinda iwe timu na hata tukipoteza ni kwa ajili ya timu na hata tuchukue mataji ni timu, siyo mtu mmoja.
Kama tuzo za binafsi ni zile za mwisho ambazo zinatolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).“Lakini vilevile anaweza kutumika kwenye mechi zetu zinazokuja mbele na wengine wakakaa tu nje,” alimaliza Mbelgiji huyo.