Katika Jimbo la Mbeya Mjini, licha ya kuwepo vyama vingi, majina mawili yanatajwa katika kinyang’anyiro cha ubunge mkoani hapo.
Jina la Tulia Ackson Mwansasu, aliyezaliwa Novemba 23, 1976 wilayani Rungwe mkoani Mbeya, yeye ni mgombea wa CCM na aliwahi kuwa naibu Spika wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania. Lakini pia, lipo jina la Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, aliyemaliza muda wake, lakini anagombea tena kupitia Chadema.
DKT. TULIA
Dkt. Tulia anasema amejipanga kunyakua Jimbo la Mbeya Mjini mwaka 2020, ili awatumikie wananchi. Akiongea na safu hii hivi karibuni, Dkt. Tulia anasema akiwa mkoani Mbeya, ameshiriki mambo mengi ya kimaendeleo ikiwemo uzinduzi wa wiki ya Chama cha Akiba na Mikopo cha Lulu Saccoss, ambapo kupitia harakati zake mbalimbali, Chama hicho kimekusanya zaidi ya shilingi milioni 11, kwa malengo ya kuisaidia na kuiinua jamii.
Anasema yeye ni miongoni mwa wadau wa elimu, hivyo atashughulikia elimu, kwani aliwahi kuwekeza katika elimu kwa kukarabati miundombinu ya Shule ya Wasichana Loleza iliyopo jijini Mbeya, ambayo naye amepata kusoma hapo.
Dkt. Tulia anasema alijiunga kidato cha kwanza katika shule hiyo mwaka 1991 akitokea Shule ya Msingi Mabonde na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1994.
Alisoma hapo hadi alipohitimu kidato cha nne, ambapo alikuwa akilala katika bweni la Mapinduzi ambalo kwa sasa limebadilishwa jina na kuitwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, mara baada ya kulikarabati.
Anaeleza kuwa, ameamua kuwekeza katika elimu kutokana na Serikali kuwa na mzigo mzito wa kutoa elimu bure kwa wanafunzi wake, hivyo naye amesukumwa kukarabati baadhi ya shule ambazo miundombinu yake si mizuri.
Anasema Serikali inatekeleza sera ya elimu bila malipo, ambapo wadau wa maendeleo, wanatakiwa kuiunga mkono sera hiyo kwa kujitolea katika mambo mbalimbali.
Dkt. Tulia anasema ameamua kukarabati mabweni mawili ya shule hiyo, pamoja na baadhi ya vyoo, baada ya kuona wanafunzi wanalala zaidi ya idadi inayotakiwa, huku baadhi ya mabweni hayo yakiwa yamefungwa kutokana na uchakavu.
Anasema licha ya mabweni hayo kuwa machakavu, pia yalikuwa hatarishi kwa wanafunzi waliokuwa wakiyatumia. “Wakati nasoma, nilikuwa nalala kwenye bweni la Mapinduzi, lakini nilipokuja kutembelea shule, nilikuta limefungwa kwa muda wa miaka saba kutokana na uchakavu, nikaamua kuanza kulikarabati na sasa bweni hilo lipo safi na limebadilishwa jina na kuitwa Dkt. Tulia Ackson,” anasema.
Dkt. Tulia anasema kuwekeza katika elimu, ni sawa na kupanda miti ambayo inafanya wananchi waweze kuvuta hewa safi na kufanya kazi zao za kulijenga taifa wakiwa na afya njema. Amewaahidi wapiga kura waje kufanya makubwa zaidi, mara watakapompa kura Oktoba 28 mwaka huu, wakati wa uchaguzi mkuu.
Kuhusu Rais John Pombe Magufuli, Dkt. Tulia amesema hakuna haja ya kutumia misuli kumpa kura rais huyo na ni vema wapiga kura watimize ule usemi wa mafiga matatu yaani rais, mbunge na diwani. Baadhi ya maswali kati ya mwandishi na Dkt. Tulia ni haya yafuatayo:
Mwandishi: Rais Magufuli ana ari kubwa ya kutaka kukabili kero za Watanzania, unadhani kama utachaguliwa Bunge lijalo, uko tayari kumsaidia kutimiza azma hiyo?
Dkt. Tulia: Mimi nadhani litamsaidia. Matarajio hayo ya wananchi si tu kwa serikali, lakini pia ni kwa wawakilishi wao waliowatuma.
Wanajua kabisa kwamba, kumfikia Rais wamueleze matatizo yao, ni ngumu, lakini wanatumia mwakilishi wao ayafikishe.
Mwakilishi amesikia mwelekeo wa serikali kuhusu afya, elimu, na kuhusu mambo yote, mbunge huyu huyu atasimama asubiri kwenye afya bajeti inasemaje, inanifikia au hainifikii.
Kwa hiyo, ninaamini Bunge hili litajiweka vizuri kwa ajili ya zile ahadi tutakazoahidi kwa wapigakura wetu.
Mwandishi: Kumekuwa na mazoea ya kutunga sheria na baada ya muda mfupi, zinarejeshwa tena bungeni kufanyiwa marekebisho.
Ukichaguliwa, utalisaidiaje Bunge kutunga sheria ambazo zinaishi muda mrefu bila kulazimika kubadilishwa mara kwa mara?
Dkt. Tulia: Kimsingi marekebisho ya sheria yanatokea siku zote na sababu zake zipo, moja inaweza kuwa ni hiyo, kwamba wakati wa kutunga kuna jambo hawakuliona vizuri au waliliona kwa namna tofauti, lakini baadaye utekelezaji wa sheria umeleta shida.
Jingine ni sheria kubadilishwa kutokana na mazingira. Pengine mazingira yamebadilika, lazima sheria iendane na mabadiliko hayo, jambo ambalo halikuwa kosa mwaka jana, mwaka huu unaweza kulifanya kuwa kosa kwa sababu ya mazingira yaliyotokea.
Kwa mfano, kuna mambo mengi yanasemwa kuhusu ile Sheria ya Makosa ya Mtandao. Kuna mambo ambayo unaweza kusema hapa kidogo utekelezaji wake ni shida, lakini yako mazuri mle, kwa hiyo huwezi kusema sheria yote ni mbaya.
Inapotokea katika utekelezaji kwamba, hili jambo litiliwe mkazo, hili liondolewe kabisa kwa sababu wananchi wanaonewa, linaondolewa. Kwa hiyo mabadiliko ya sheria katika hii tasnia ya sheria, huwa ni ya kawaida sana.
Hata Katiba, ndiyo maana huwa inabadilishwa muda kwa muda, kutegemea jambo lenyewe mnataka kubadilisha kwa sababu gani.
Mwandishi: Katika kutimiza vipaumbele vya Rais, kunaweza kutokea usaliti, unadhani ukichaguliwa, Bunge litamsaidia vipi hali hiyo ikianza kutokea?
Dkt. Tulia: Rais ameahidi kupasua majipu, Bunge litamsaidia kwa maana ya kushirikiana naye na kama alivyosema, ametaja sheria chache, lakini ziko sheria nyingi zitakazopaswa kubadilishwa ama nyingine kutungwa ili kuweza kuyafanya yale yote aliyoyasema, si yote kwamba sheria ipo na itaunga mkono namna yeye anavyotaka kwenda.
Kwa hiyo, sisi tukichaguliwa, tutamuunga mkono kwa kuweka mazingira ambayo serikali inaweza kuyafanyia kazi kwa sababu serikali haiwezi kufanya jambo ambalo halijatungiwa sheria na Bunge.
Umeuliza kuhusu usaliti, mimi ningependa kuamini kwamba watu wataangalia mwelekeo wa Rais ni upi, kwa hiyo ule usaliti wao lazima tu utadhibitiwa.
Naamini watamwelewa Rais na watafanya yale ambayo ameagiza. Kama mtu anajishughulisha na dawa za kulevya, ataacha kwa sababu rais yuko serious, kama mtu anafanya ufisadi ataacha.
SUGU
Naye aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini; Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, alizaliwa Mei Mosi, 1972 katika Hospitali ya Ligula, Mtwara.
Mwaka 2010 aliingia rasmi kwenye siasa baada ya kuchukua kadi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kugombea ubunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, akashinda na kufanikiwa kuingia bungeni, ambako alikuwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Sugu anasema mwaka huu, atashinda tena katika kinyang’anyiro, kwa sababu chama chake kimefanya vema jimboni humo licha ya kufanyiwa figisufigisu.
“Wagombea Ubunge na Kata (Madiwani), wamekaa kwa muda mrefu Dodoma kufuatilia rufaa zao. Nimeenda Dodoma kuwaeleza ni uhuni gani umefanyika huko chini,” anasema Sugu.
“Nashangaa kuona majimbo 18 yamepita bila kupingwa, wakati kuna majimbo ya vyama kadhaa wamekata rufaa, sasa wanasemaje yamepitwa bila kupingwa?” Alihoji Sugu.
Jiji la Mbeya limeongozwa na Sugu na limekua likitajwa kama mojawapo ya ngome Chadema.
Dkt Ackson Tulia (BI Khadijah) ndiyo Habari ya Mjini.
ReplyDeleteJOSEFU MBINYI aendelee na Reception hotelini.
Wana Mbeya TUNATAKA waleta MAENDELEO na siyo WA disco