Mke wa King Kiki awaonya wanaojidai wasemaji wa familia



COSTANSIA Kalanda ambaye ni mke wa msanii muziki wa dansi nchini Tanzania, King Kiki, amefunguka kuhusu kuumwa kwa mumewe huyo huku akiwaonya wanaochukuwa jukumu la kuzungumzia afya ya mumewe.


King Kiki ni mmiliki wa bendi ya La Capital, inayotesa na mtindo wake wa Kitambaa Cheupe.


Habari za kuumwa kwa King Kiki zilizagaa wiki iliyopita  zikimuonyesha akiwa katika picha na familia yake kitandani  wakimpa msaada wa kukaa.



 

Taarifa hizo zilisema “Anaumwa yuko kitandani mwanamuziki nguli  anahitaji msaada wa hali na mali. Alikuwa anaumwa mgongo na baadae kupooza alilazwa Muhimbili gharama zikawa kubwa sasa uanugulia nyumbani kwake,”.


Akizungumzia jambo hilo, mke wa msanii huyo Costansia, amesema taarifa za kuwa mume wake anaumwa ni za kweli japokuwa amekanusha kuwa familia haijashindwa kumuhudumia kimatibabu.


“Ni kweli King Kiki anaumwa, lakini taarifa kuwa ametoka hospitali kwa kushindwa kumudu gharama za matibabu hazina ukweli wowote kwani familia tupo tunamuhudumia,”amesema.


Akizungumzia kuhusu ugonjwa unamsumbua, Costansia amesema alipata tatizo la uti wa mgongo kama mwezi mmoja uliopita na kufanyiwa upasuaji wa pingili za shingo wiki mbili zilizopita.


Amesema kutokana na upasuaji huo alijikuta akishindwa kunyanyuka na kukaa mwenyewe kutokana na madhara aliyopata wakati wa kuwekewa ganzi.


“Madaktari wametumbia kwa kuwa kutokana na King Kiki kuwa mtu mtu mzima ilibidi wampige ganzi ile ya kuuwa mwili mzima wakati wa kumfanyia upasuaji.


“Ni kutokana na hilo walisema ingemchukua takribani wiki mbili kurudi katika hali yake ya kawaida na mpaka tunafika leo wiki mbili hizo tayari zimefika, hapa tunafanya utaratibu kesho tumrudishe hospitali kwa uchunguzi zaidi," amesema Costansia.


Hata hivyo amewaonya watu wanajitwika usemaji wa familia kwa kumzungumzia msanii huyo  na kusema kwamba wanaopaswa kufanya hivyo ni yeye na mtoto wake mkubwa wa kiume.


Pia aliwaondoa hofu mashabiki wa msanii huyo na kueleza kuwa hayupo katika hali mbaya kihivyo kama inavyosemwa huku akiwaomba wamuombee  ili aweze kunyanyuka na kuendelea na kazi zake za sanaa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad