Mgombea Ubunge jimbo la Singida mjini kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Sima amewataka Watanzania kupuuza wapinzani wanaombeza Rais Dk. John Magufuli kutokana na jitihada alizozifanya za kuiongoza Tanzania kupiga hatua kubwa kimaendeleo.
Sima ametoa kauli hiyo jana wakati akihutubia wananchi wa jimbo hilo na kuwaomba wampe ridhaa ya kipindi cha pili ili kuendelea kuifanya Tanzania kuwa nchi za mfano.
Alisema katika uongozi wake Rais Magufuli ameonesha kuwa ni mwaminifu, kiongozi wa wanyonge, mtiifu, mtumishi na mwenye maono kuliko rais yeyote duniani.
“Mimi nilipewa heshima ya kipekee ikiwamo wanaSindiga wote na wana Kindai kunitea kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
“Mlivyonichagua, Rais akasema namhitaji zaidi kunisaidia kazi na kumsaidia Mama Samia, Mama yetu ambaye kama mnavyojua ni muadilifu. Tumefanya naye kazi vizuri na bado anaendelea kutuamini. Hii yote ni kwa sababu ya heshima yenu.
“Nataka niwaeleze ndugu zangu, tuko kwenye uchaguzi yanasemwa mambo mengi na wapinzani, wanabeza tuliyoyafanya, lakini cha kusikitisha zaidi wanambeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania. Na wanawapotosha watanzania,” alisema.
Alisema kwa kuwa jikoni ameona mambo mengine ambayo wapinzani wanayatumia kuwapotosha watanzania.
“Nataka niwakumbushe kuwa tumepata fedha Sh bilioni 32 na bado mradi wa Ziwa Victoria utapita hapa Singida. Haya maji yote nawaambia ndugu zangu, sisi tunahitaji kutengeneza kiwanda cha maji, si kuhitaji tena maji ya kutumia.
“Kazi kubwa mnayonituma ni kuifanya Singida kuwa jiji. Sasa hao wanaokuja leo wanataka kutupeleka wapi kama sio kuturudisha nyuma?
“Hadhi ya Dodoma mnayoiona haiwezi kuwa Singida leo. Tulikuwa na barabara za lami km 11 lakini sasa tuna km 19.5, kazi mnayonituma leo ni kuhakikisha Tarura inapata fedha ya kutosha ili kuhakikisha tunakamilisha barabara zetu za mtaani na hayupo mwingine ni mimi,” alisema.