TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya, inamshikilia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyeregete iliyoko wilayani Mbarali, Adelhard Mjingo (44), kwa tuhuma za kuomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 14.
Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake leo Septemba 25,2020, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Julieth Matechi, amesema mwalimu huyo alinaswa na makachero wa taasisi hiyo, Septemba 23 mwaka huu akiwa na mwanafunzi huyo kwenye moja ya nyumba za kulala wageni kwa lengo la kutekeleza tukio hilo kwa ahadi ya kumsaidia kufaulu mitihani.
Amesema taasisi hiyo ilipata taarifa za siri kutoka kwa mmoja wa wananchi kuwa mwalimu huyo amekuwa akiomba rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wake huyo huku akimsisitizia kuwa endapo angekataa, angehakikisha anamfelisha kwenye mtihani wake wa mwisho.
Matechi amesema, siku ya tukio mwalimu huyo aliaga shuleni kuwa anaenda kwenye semina ya chanjo katika Mji wa Rujewa wilayani humo na aliondoka pamoja na walimu wenzake lakini alipofika kwenye ukumbi aliandikisha jina na kuomba udhuru kisha akaondoka kwenda kukutana na mwanafunzi huyo kwa lengo la kutekeleza tukio lake na ndipo makachero wa TAKUKURU walipofanikiwa kumnasa kabla ya kutenda tukio hilo.