Mwanafunzi Atiwa Mbaroni Kwa Kumkata Mapanga Mwalimu Wake



Mwanafunzi  wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Kiaga wilayani Butiama, mkoani Mara, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumkata mapanga na kumsababishia majeraha mwalimu. 

Inadaiwa kuwa chanzo ni utoro shuleni na kuamriwa kuita wazazi shuleni. 


Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Daniel Shillah, alisema tukio hilo limetokea shuleni majira ya asubuhi wakati mwalimu akiwa anakagua wanafunzi watoro ndipo mwanafunzi huyo alimkata panga mwalimu wake wakiwa darasani. 


Alisema mwanafunzi huyo amekuwa na tabia ya kutodhuria shuleni mara kwa mara, jambo ambalo liliwalazimu walimu kumuandikia barua ya kuita wazazi ili wajue sababu za kutohudhuria mara kwa mara. 


Shillah aliongeza kuwa wakati mwalimu huyo akikagua wanafunzi watoro darasani, alimuuliza mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa) sababu ya kutokuja na wazazi wake, ndipo alipochomoa panga alilokuwa amelificha ndani ya nguo zake za shule na kuanza kumkatakata mwalimu sehemu ya bega la kulia na kiganja cha mkono wa kushoto. 


Kamanda huyo alisema walifanikiwa kumtia mbaroni mwanafunzi huyo, na kuwa yupo mahabusu akisubiri uchunguzi kukamilika ili afikishwe mkortini. 



Mwalimu huyo, Majogoro John, alisema wakati anaita majina ya wanafunzi watoro darasani hapo alimuona mwanafunzi huyo na kumuuliza kwanini hakuchukua barua ya kupeleka kwa wazazi wake, lakini mwanafunzi huyo hakumjibu kitu, badala yake akasubiria wakati anatoka darasani ndipo akachomoa panga alilokuwa na kuanza kumkatakata. 


Alisema alipoona mwanafunzi huyo anamsogelea akamgeukia na kukatwa panga la begani upande wa kulia na kwamba wakati anajiandaa kukabiliana nae, akamkata tena kwenye kiganja cha mkono wa kushoto ukawa unaning’inia kisha mtuhumiwa alikimbia kutoka eneo la tukio. 



Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mara, Dk. Joachim Iyembe, amesema walimpokea majeruhi huyo na kumfanyia uchunguzi wa awali na kubaini kuwa sehemu iliyojeruhiwa zaidi ni mkono wa kushoto ambapo mifupa miwili imekatika na kusababisha mishipa ya fahamu kutokufanya kazi . 


Iyembe alisema kuwa kutokana na kuhitaji huduma za matibabu zaidi hospitali ya mkoa imeamua kumpa rufani ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. 


Nayo ofisi ya mkuu wa mkoa imetoa tiketi ya ndege kwa ajili ya mwalimu huyo kupelekwa Muhimbili jijini Dar es Salaam haraka, huku hospitali ya mkoa ikitoa gari kwa ajili ya kumfikisha mgonjwa huyo jijini Mwanza kwa ajili ya kupanda ndege.

 




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad