Alexei Navalny, mpinzani mkuu wa rais wa Urusi Vladimir Putin, ametoka katika hali ya nusu kaputi na anaweza kusikia, hayo ni kulingana na maelezo ya hospitali ya Charite anakotibiwa mjini Berlin.
Serikali ya Ujerumani imesema kuwa kiongozi huyo wa upinzani nchini Urusi alipewa sumu ya kiwango cha kivita ya Novichok.
Taarifa ya hospitali hiyo imesema hali ya mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 44 imeboreka kiasi cha kuwaruhusu madaktari kumuondoa katika hali ya nusu kaputi, na kumuondoa hatua kwa hatua katika mashine za kumsaidia kupumua.
Hospitali hiyo imeongeza katika taarifa yake kuwa haiwezi kuondoa uwezekano wa athari mbaya na za muda mrefu za sumu hiyo katika mwili wa Navalny.