Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole, amewaonya viongozi na wagombea wa nafasi mbalimbali katika chama hicho wajiepushe na siasa za kusema watu badala yake wajikite kufanya siasa zenye kuzingatia ustaarabu.
Amesema hayo leo Agosti 31, 2020, wakati akitaja majina ya wagombea wa uwakilishi kwa upande wa Zanzibar na kusema kuwa kwa upande wa Tanzania Bara wamezindua kampeni zao vizuri kwa kuwasilisha hoja zao kwa Watanzania.
"Tufanye siasa za kistaarabu,na sisi tumezindua kampeni juzi vizuri kabisa hatutaki kusema watu ,tunasema hoja tunaziwekea sababu na tunaeleza tunachotaka kupeleka kwa watanzania", amesema Polepole
Akimzungumizia mgombea Urais kwa upande wa Zanzibar Polepole amesema, "Tumempata mtu mmoja mpole,mtaratibu, mtu wa watu, mwenye nidhamu ya hali ya juu ambaye amehudumu kwenye dhamana ya uongozi kama kiongozi mwandamizi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ni Mzanzibari kwelikweli ndugu yetu Hussein Mwinyi”.