Mamlaka katika mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abu Dhabi imeondoa masharti ya kupata kibali cha kununua na kunywa pombe, baada ya mji jirani wa Dubai kuchukua hatua kama hiyo.
Ulegezaji huo wa masharti katika miji hiyo unalenga kuikuza upya sekta ya utalii ambayo imeathiriwa vibaya na janga la virusi vya corona, na kujiandaa kuwapokea watalii kutoka Israel baada ya kuwekeana uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo.
Barua kutoka idara ya utamaduni ya mji wa Abu Dhabi imesema kuanzia sasa, wenyeji na wageni katika mji huo wataweza kununua pombe kutoka maduka yaliyoruhusiwa, bila kuhitaji vibali maalumu.
Barua hiyo inasema pombe itakayonunuliwa sharti inywewe majumbani, au mahali palipoporuhusiwa kama vile kwenye baa.