Mfalme Salman wa Saudi Arabia amewafuta kazi watu wawili wa familia ya Kifalme na akawaweka chini ya uchunguzi wa ufisadi katika wizara ya ulinzi pamoja na maafisa wengine wanne wa kijeshi.
Amri hiyo ya Mfalme Salman imesema Mwanamfalme Fahd bin Turki Abdulaziz Al Saudi ataondolewa kwenye wadhifa wake wa kamanda wa majeshi ya pamoja katika muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita nchini Yemen, na mtoto wake wa kiume Mwanamfalme Abdulaziz bin Fahd ameondolewa kwenye nafasi yake ya naibu gavana wa jimbo la al-Jouf.
Uamuzi huo umetokana na barua ya Mrithi wa kiti cha Ufalme Mohammed bin Salman kwa kamati ya kupambana na ufisadi ya kuitaka ichunguze shughuli za kifedha zinazotiliwa shaka katika wizara ya ulinzi.
Mwanamfalme Salman amelipa kipau mbele suala la vita dhidi ya rushwa katika mageuzi anayoyafanya nchini humo.